
KLABU ya Simba jana ilifanikiwa kuichapa JKT Tanzania bao 1-0 kwenye mchezo wa Raundi ya Tatu ya
Kombe la Azam Sports Federation Cup (FA), uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar.
Bao la dakika ya 27 kipindi cha kwanza la Kubu Denis aliyeunganisha pasi ndefu ya beki wa kati wa Simba, Pascal Wawa, iliwapa tiketi Simba ya kutinga hatua ya 32 bora.
Simba ambao ni mabingwa watetezi wa kombe hilo, walifanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chao
kwa kuwapa nafasi wachezaji ambao hawakuwa wakipata nafasi kwenye ligi.

Ambapo safu ya mbele ilijengwa na Kibu Denis, Peter Banda na Ousmane Sakho. Safu ya ulinzi ilikuwa na kipa Beno Kakolanya, Gadiel Michael na Israel Mwenda. Duncan Nyoni, Jimson Mwinuke, Yusuphu Mhilu
na Ibrahim Ajib nao walipata nafasi ya kucheza.
Mchezo ulikuwa wazi toka kipindi cha kwanza kufuatia JKT Tanzania kucheza kwa kufunguka kwa
wakati wote na wakionyesha hamu ya kutaka kupata ushindi.

Kipindi cha pili Simba walikuwa moto zaidi baada ya Maddie Kagere, Mwinuke kuingia ambapo kwa kiasi fulani lango la JKT lilikuwa kwenye wakati mgumu zaidi. Baada ya Simba kutengeneza mashambulizi matatu ya hatari ambayo moja kati ya hilo liligonga mwamba na mengine mawili yakizalisha kona.
Matokeo mengine ya michuano hiyo, Dodoma Jiji iliwachapa Pan African mabao 2-0. Leo kutakuwa na michezo miwili ambapo Azam FC watacheza na Green warriors saa 10:00 jioni na Yanga itavaa na Ihefu saa 1:00 usiku.
STORI NA ISSA LIPONDA | CHAMP[IONI JUMATANO