
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula leo Desemba 16, 2021 amewasili nchini Uturuki kwa ajili ya kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Afrika na Serikali ya Uturuki utakaofanyika jijini Istanbul kuanzia leo hadi Desemba 18, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano katika wizara hiyo, Emmanuel Buhohela, Balozi Mulamula ambaye pia anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo, anatarajiwa kuhutubia Desemba 18, 2021 ambapo atawasilisha ajenda za Tanzania zenye manufaa kwa nchi kupitia ushirikiano huo ambazo ni pamoja na fursa za elimu kwa Watanzania, kilimo, ujenzi na Uchukuzi.
Mkutano huo ambao unafanyika kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa kwa ushirikiano kati ya nchi za Afrika na Uturuki mwaka 2008, unalenga pamoja na mambo mengine kufuatilia utekelezaji wa makubaliano na maamuzi mbalimbali yaliyopitishwa na wakuu wa nchi kwenye mikutano iliyopita na kujadili pamoja na namna ya kuimarisha uhusiano huo.