
Meneja wa Manchester City Pep Guardiola amemlinganisha Sergio Aguero na wababe wa Argentina Diego Maradona na Lionel Messi baada ya mshambuliaji huyo wa Barcelona kutangaza kustaafu Jumatano akiwa na umri wa miaka 33 kutokana na ugonjwa wa moyo.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa City, alifunga zaidi ya mabao 400 katika kipindi chake cha miaka 18 na pia alichezea Atletico Madrid na Independiente. Aliichezea Argentina mechi 101.
“Maradona aliishinda Italia, Messi alifanya hivyo Uhispania na Aguero amefanya hivyo huko Uingereza, idadi yake inajieleza,” Guardiola aliiambia ESPN Argentina.
Aguero aliisaidia Argentina kushinda Copa America 2021 – taji lao la kwanza kuu ndani ya miaka 28 – na Messi alitoa pongezi kwa mshambuliaji huyo kwenye ukurasa wake wa Instagram.
“Ukweli sasa inauma sana kuona ni kwa jinsi gani unapaswa kuacha kufanya kile ambacho unakipenda zaidi kwa sababu ya kile Kilichotokea kwako,” Messi alisema.
“Tuliishi nyakati nzuri sana na zingine ambazo hazikuwa nyingi, zote zilitufanya kuwa na umoja zaidi na zaidi. Tutaendelea kuishi pamoja nje ya dimba.”