×

Wazazi wa Nandy Wamkubali Nenga

ILIKUWA ni miaka mitano ya mapenzi na uchumba uliogubikwa na milima na mabonde tangu mwaka 2016, lakini hatimaye wazazi wa Malkia wa Bongo Fleva, Faustina Charles almaarufu Nandy wamemkubali mchumba’ke, William Lyimo au Billnass na sasa ndoa inanukia.

 

Katika kipindi chote hicho cha mapenzi yao, Nandy au Nandera na Billnass au Nenga waliripotiwa mara wameachana na mara wamerudiana.

 

KAPO MAARUFU ZAIDI

Wawili hao ambao ni mojawapo ya kapo maarufu iliyojizolea mashabiki wengi Bongo, wanadaiwa kuwa kwenye mipango ya ndoa ikiwa ni miezi michache baada ya Billnass kumtolea posa na kumvisha Nandy pete ya uchumba kwa mara nyingine baada ya ile ya mwanzo kusemekana ilipotea!

 

Nandy na Billnass wamedumu kwenye uhusiano kwa muda mrefu huku wakipita kwenye vipindi vya in and out (kuingia na kutoka) kutokana na sababu kadha wa kadha.

 

MADAI YA NENGA KUKATALIWA UKWENI

Miongoni mwa sababu hizo, yapo madai kwamba, upande wa Nandy; yaani ukweni au wazazi na baadhi ya ndugu hawakuwa wakimkubali Nenga awe mkwe au shemeji yao, lakini sasa wamekubali muziki na posa ya jamaa huyo.

 

Hata hivyo, kuhusu suala la kukataliwa ukweni, Nenga aliwahi kulikanusha akisema; “Sidhani kama ni kweli, lakini pia wakwe zangu mimi ni watu wa dini sana, hivyo nisingependa kuwaongelea sana kwenye media yoyote ile kwa sababu ninachokijua mimi ni kwamba, wananipenda kama mtoto wao na wamenikubali.”

 

Habari za ndani zinaeleza kwamba, kwa sasa kopa la wawili hao limejaa upya baada ya kwenda kujiachia Dubai kisha kurejea kwa wazazi wa Nandy ambapo Nenga alionekana akiwa amepiga picha na baba na mama wa mpenzi wake huyo, jambo ambalo awali halikuwahi kutokea.

 

Kabla ya kusambaa kwa picha ya Nenga na wazazi wa Nandy, jamaa huyo aliposti picha kwenye ukurasa wake ikimuonesha mrembo huyo na mama wa jamaa huyo na kuandika; “My Mommy and her best friend! Mtu na mkwe wake! Naipenda sana hii picha na nawapenda sana walioko kwenye hii picha Inshaalah kuna siku nitawaongezea rafiki yao mwingine nitakayempenda zaidi…”

 

MIMBA YATAJWA

Huyu rafiki mwingine inasemekana tayari Nandy ni mjamzito ndiyo maana hata aina za picha anazopiga kwa sasa anaficha kitumbo chake kama alivyofanya kwenye Shoo ya Komaa Concert hivi karibuni kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers vilivyopo Kawe jijini Dar, hivi karibuni.

 

Chanzo cha karibu na wawilin hao kinasema kuwa, ndoa ya Nandy na Nenga inatarajiwa kufungwa mapema mwakani kwani wazazi wa mrembo huwa wasingependa mtoto wao huyo akajifungua mtoto wan je ya ndoa.

 

WAMETOKA MBALI

Wawili hao waliwahi kuliambia gazeti hili kwamba, kwa mara ya kwanza waliandika ukurasa wao wa mapenzi wakiwa ziara ya Tamasha la Fiesta lililofanyika mkoani Mbeya mwaka 2016.

STORI; SIFAEL PAUL, DAR

Leave a Comment