
HATIMAYE Kocha Mkuu wa Simba raia wa Hispania, Pablo Franco ameshusha presha yake baada ya straika wake Mkongo, Chris Mugalu kuimalika na kuunganishwa katika kikosi kilichoenda mjini Bukoba kupambana na Kagera Sugar.
Kesho Simba itashuka katika Uwanja wa Kaitaba, kupambana na Kagera Sugar, ikiwa ni mchezo wao wa tisa wa
Ligi Kuu Bara, baada ya kuvuna pointi 18 katika michezo nane iliyopita na wapo nafasi ya pili.
Chanzo chetu kutoka Simba, kimeliambia Championi Ijumaa kwamba, tabasamu la Pablo limeongezeka baada
ya kushuhudia uimara wa Mugalu ambaye alikuwa nje ya dimba kwa takribani mwezi mmoja akiuguza
majeraha ambayo kwa sasa yamepona na yupo katika kikosi kilichopo Kagera.
“Pamoja na kocha Pablo kuendelea kuona uwezo mzuri wa washambuliaji aliowakuta kikosi, bado alikuwa akisisitiza zaidi kuona straika wakiongezeka ili awe na kikosi kipana jambo ambalo ni faraja kubwa kwake kwa sasa.
“Mugalu kapona na ameanza mazoezi na wenzake na katika mipango ya mwisho ya kocha naye alikuwa ni
miongoni mwa nyota wanaoenda Kagera kupambana hivyo, kama hatabadilisha uamuzi maana yake atakuwa sehemu ya kikosi hicho,” kilisema chanzo hicho.
STORI: MUSA MATEJA, Dar es Salaam