
SERIKALI imesema haina taarifa za kushikiliwa kwa meli ya mizigo iliyobeba taka za nyuklia nchini Kenya ambayo iliripotiwa kuwa njiani kuelekea Tanzania, lakini itazifuatilia.
“Hatujapokea taarifa zozote kuhusu meli hiyo, lakini nitawasiliana na mamlaka husika kwa maelezo yoyote kuhusu suala hilo,” alisema Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Gabriel Migire alipozungumza na gazeti hili kuhusu suala hilo, na kuongeza kuwa meli yoyote itakayofika Tanzania inatakiwa kupeperusha bendera ya nchi.
Vyombo vya habari vya Kenya viliripoti jana kuwa meli hiyo ilitia nanga katika bandari ya Mombasa, ikiwa imesheheni taka hatari za nyuklia ambazo zilipaswa kutupwa katika pwani ya Afrika Mashariki, na hivyo kuhatarisha afya za mamilioni ya watu katika eneo hilo.
Shehena iliyokuwamo kwenye meli ya MV Piraeus Voy ilifanywa ionekane kama shehena ya makufuli na vifaa vingine vya ujenzi, na ilizuiliwa baada ya Wizara ya Afya ya Kenya kutoa tahadhari kwamba ilikuwa imebeba nyenzo za mionzi.
Maofisa wanaochunguza suala hilo, walisema meli hiyo ilisafiri hadi Kenya ikitokea Mumbai, India na ilikuwa ikielekea nchi jirani ya Tanzania. “Hii ni njia dhahiri ya kutupa vitu hatari katika Afrika Mashariki.
Tunao ushahidi kuwa kilichotangazwa ni sehemu tu ya yaliyomo, lakini madini ya mionzi nayo yamo ndani ya meli na yanatoa mionzi mikali,” chanzo kinachohusika na uchunguzi unaoendelea kilisema kwa sharti la kutotajwa jina kwa kuwa hakina mamlaka ya kuzungumza na vyombo vya habari.
Viwango vya juu vya mionzi inayotokana na taka za nyuklia inaweza kusababisha athari mbaya za kiafya kama vile kuungua ngozi. Inaweza pia kusababisha athari za kiafya za muda mrefu kama saratani, ugonjwa wa moyo na mishipa.
Timu ya mawakala inayojumuisha maofisa kutoka mashirika mbalimbali ya Serikali katika bandari ya Mombasa imetofautiana kuhusu namna bora ya kuihudumia shehena hiyo.
“Baadhi ya walioko kwenye timu hiyo wanataka shehena hiyo irudishwe kwa mtumaji kwa mujibu wa sheria za baharini, lakini wapo wanaopendekeza tuachie meli ili ielekee Tanzania, au tuifanyie vipimo zaidi mizigo hiyo.
Wasiwasi wetu ni kwamba, ikiwa tutaiachia shehena hiyo mamlaka katika nchi inakokwenda inaweza kukosa uwezo wa kutosha wa kugundua au kutupa taka, na hivyo kuwaweka watu kwenye hatari.
Tusubiri tuone kitakachotokea,” kilisema chanzo hicho. Meli hiyo inasemekana katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita ilisafiri kwenda Kenya, Oman, India na Pakistan. Tovuti ya ufuatiliaji meli, inaonyesha kuwa meli hiyo ilikuwa Mumbai, India Desemba 2 mwaka huu.
Mamlaka ya Kudhibiti Nyuklia nchini Kenya (KNRA) jana ilithibitisha kuwa meli hiyo ipo salama mjini Mombasa, baada ya wiki iliyopita Waziri wa Afya Mutahi Kagwe aliamuru izuiwe.
Mkurugenzi mkuu wa KNRA, Joseph Maina alisema mamlaka hiyo inaongoza ukaguzi na uhakiki wa kontena iliyo kwenye meli ya MV Seago Piraeus Voy.
“Tupo katika mchakato wa kuamua ikiwa tutakusanya sampuli ili kubaini kitu (dutu) halisi baada ya kugundua kuwa kuna vifaa vya mionzi kwenye shehena au kurudisha shehena kwa mtumaji. Serikali ya Kenya ilisema itawalazimisha waliomo ndani ya meli hiyo kujibu swali lolote kulingana na vifungu vya 60 na 62 vya Sheria ya afya ya umma.