
WATOTO Yatima na wenye uhitaji maalum wa Kituo cha Mama wa Huruma kilichopo Madale, Dar wamefanyiwa sapraiz na Kampuni ya Najuna General Supplies Ltd kwa kupelekewa vitu mbalimbali kama vile vyakula, mafuta ya kupakaa, dawa za meno, miswaki, vinywaji, sabuni, nguo mpya na vitu vingine vingi pamoja na shilingi million tano.

Akikabidhi vitu hivyo baada ya ibada fupi iliyofanyika kwenye kituo hicho kinachoongozwa na Sister Christina Christopher, Mkurugenzi wa Kampuni ya Najuna General Supplies, Gadi Mjuni Kalugendo amesema kampuni hiyo imetoa vitu hivyo kama sadaka waliyomtolea Mwenyezi Mungu kupitia watoto hao.

Kalugenzo amesema baada ya kufanyakazi kwa mwaka mzima huku Mungu akiwapigania hatua kwa hatua wameona ni vyema kumshukuru Mungu katika kipindi hiki cha kuelekea Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya.
“Mungu ametupigania katika afya zetu na mambo mengine katika kipindi chote hiki mpaka sasa hivyo hatuna budi kumshukuru kwa kutoa sadaka kidogo kwa watoto yatiba na wenye uhitaji”, amesema Mkurugenzi Kalugendo.

Baada kutoa sadaka hiyo mlezi wa kituo hicho, Sister Christina alielezea changamoto za kituo hicho ambapo kubwa ni deni la milioni 20 wanalodaiwa na aliyewapa kiwanja walipojenga kituo hicho.
Sister Christina alisema tayari Wasamaria Wema wameshawachangia shilingili milioni nane ambapo baada ya kumaliza kauli hiyo, Mkurugenzi Kalugendo naye hapohapo aliahidi kuwapa shilingi milioni tano.
Kampuni hiyo yenye Makao Makuu yake Jengo la Posta Ghorofa ya 9, Jiji Dar inajihusisha na uuzaji wa vifaa vya kupambana na moto, sare za kiofisi, upuliziaji dawa kwa wadudu waharibifu na shughuli nyinginezo. HABARI/PICHA: RICHARD BUKOS /GPL