
Mabasi tisa ya abiria katika stendi kuu ya mabasi ya Nyegezi jijini Mwanza yang’olewa namba na kuzuiwa kuendelea na safari baada ya kubainika kuwa ni mabovu kupitia ukaguzi ulioongozwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Wilbroad Mutafungwa.
Kamishna Mutafungwa ameyazuia mabasi hayo tisa kutoka kampuni tofauti kufanya safari asubuhi ya leo kutokana na kile kinachodaiwa kukosa vigezo vya kiusalama kufanya safari hizo.
Kamanda Mutafungwa ametoa uamuzi huo wakati Kikosi cha usalama barabara nchini kikifanya ukaguzi na kukagua mabasi yanayofanya safari kati ya Mwanza na mikoa mingine ili kujiridhisha iwapo mabasi hayo ni salama kusafirisha abiria.
Sababu nyingine ni kadhia ya wasafirishaji abiria kutumia magari yanayohatarisha usalama wa wananchi, kupandisha gharama za nauli ghafla kulingana na mahitaji ya msimu wa sikukuu na baadhi ya madereva wa vyombo vya moto kufanya kazi wakiwa wamelewa.
Kamanda Mutafungwa amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na wamiliki wa magari kutotumia kipindi hiki cha msimu wa kuelekea sikukuu kinachokua na abiria wengi kuingiza magari mabovu barabarani ili wajipatie kipato.