
WAZIRI wa Ulinzi na Polisi wa Madagascar, Serge Gelle (57) ameogelea kwa saa 12 baharini hadi kufika nchi kavu baada ya helikopta aliyokuwa akifanyia doria kuanguka baharini, huku akisema haukuwa muda wake kufariki.
Gelle ambaye alikuwa polisi kwa miaka 30 kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri hivi karibuni, aliogelea kwa masaa kumi na mawili kabla ya kufika nchi kavu katika mji wa Mahambo siku ya Jumanne. Waziri huyo alitumia kiti kimoja cha helikopta kama kifaa cha kumsaidia kuelea.

Maafisa wengine wawili waliokuwa wameambatana naye pia wamenusurika na kwamba walikuwa wakikagua eneo lililoko Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo ambako kulitokea ajali ya boti ya abiria iliyoua watu wapatao 39 na wengine wengi kupotea.