
Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema jeshi la polisi limeendesha oparesheni maalum ya kuwasaka watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu ambapo watu 61 wanaotuhumiwa kujihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu wamekamatwa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda Muliro amesema miongoni mwa watuhumiwa hao, wapo watuhumiwa saba wanaoongozwa na mtuhumiwa aitwaye Yohana Zacharia almaarufu Cobra, ambao wamekuwa wakitumia bastola bandia kutishia watu na kuwapora, watu watano ni wafanyabiashara wa dawa za kulevya, 34 wanajihusisha na biashara ya bangi.
“Kumekuwa na oparesheni kali ambayo inaongozwa na taarifa fiche, zinazolenga watu wanaojihusisha na vitendo vya kufanya uhalifu na watu 61 ambao walikuwa wakijihusisha na uhalifu wamekamatwa.
“Waliokamatwa miongoni mwao ni watuhumiwa 7, ambapo kundi hili yumo mtuhumiwa anayeitwa Yohana Zacharia maarufu kama Cobra, yeye na wenzake wamekuwa wakitumia bastola bandia kutishia watu na kunyang’anya,” amesema Kamanda Muliro.
Ameongeza kuwa jeshi la polisi linaendelea na ahadi yake ya kutoa zawadi ya shilingi milioni mbili kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha majambazi wanaofanya unyang’anyi wa kutumia silaha kukamatwa.