
Baada ya Masauti kujitetea kufuatia kuvuma kwa taarifa za matatizo yaliyotokea kwenye onesho aliloalikwa kutumbuiza yeye pamoja na wasanii kadhaa akiwemo Mbosso kutoka Tanzania.
Hatimaye, mratibu wa Tamasha la Bright Future lililofanyika takribani wiki moja iliyopita huko Mombasa nchini Kenya, amesema kuwa msanii Masauti aliiaibisha Mombasa nzima kwa kitendo cha kuchelewa kutumbuiza kwa zaidi ya saa mbili.
Bianca, amefichua kuwa timu yake ilijaribu kuwasiliana na Masauti ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo yaliyotokea baada ya kufanyika kwa makosa hayo tangu siku ya tukio.
“Masauti, watu kadhaa wamekupigia lakini umekataa kupokea simu. Tafadhali fanya kinachohitajika, achana na aibu,” aliomba Bianca.
Taarifa za awali zilieleza kuwa Masauti na Nadia Mukami waliamriwa kutoka nje ya jukwaa bila ya kujali ili kutoa nafasi kwa msanii Mbosso kutoka nchini Tanzania kutumbuiza kwenye jukwaa hilo.
Hata hivyo siku ya Jumatano, Desemba 22, Masauti aliweka ujumbe kwenye ukurasa wake wa mtandao wa instagram, akimlaumu muandaaji wa onesho hilo kwa misukosuko iliyojitokeza, na kulisafisha jina la Mbosso lililokuwa likitajwa mara kwa mara.
“Sijataka kuongelea issue ya show ya Mombasa lakini pia nimeona nivunje ukimya ili kuepuka unafiki. Najua mashabiki zangu wanahofu kutaka kujua what exactly happened ndio nisingependelea mtu atumie jina langu kuelezea my side of the story.
Nataka niwaombe tu tukio hili lilitokea, lisitumike kumharibia rafiki yangu Mbosso wakati siye aliyeandaa show hii,” aliandika Masauti katika chapisho lake.