
Watu wengi hawaelewi kwamba Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA) si eneo ambalo lipo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na badala yake ni shirika huru linalojitegemea kikazi.
Majukumu ya Tanapa na Ngorongoro yanafanana katika kuhifadhi viumbe hai na makazi yake kuwa endelevu kwa ajili ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ni eneo ambalo ni hifadhi mseto ambapo kuna viumbe hai aina tatu vikiishi kwa pamoja ambavyo ni watu ambao zaidi ni jamii ya kabila la wamaasai, mifugo yao kama kondoo, mbuzi na ng’ombe na wanyamapori.

Mamlaka hii ilianzishwa mwaka 1959 na Aprili 17, 2018 ilitambuliwa na Umoja wa Matyaifa kupitia shirika lake la Elimu Sayansi na Utamaduni (Unesco) kuwa hifadhi jiolojia ya Ngorongoro Lengai hivyo kuingizwa kwenye mtandao wa hifadhi zenye hadhi hii duniani. Kijiografia inapatikana mkoani Arusha.

Sababu ya msingi iliyosababisha kuanzishwa kwa hifadhi hii ni ukweli kwamba jamii ya kabila la Wamasai ilikuwa ikiishi katika eneo la Serengeti na Ngorongoro kwa miaka mingi pamoja na wanyamapori, hivyo lengo ni kusimamia uendelevu wake kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Wamasai ni jamii ya nilotiki ambao asili yao ni kusini mwa Sudani na ni jamii ya wafugaji kiasili. Kwa kuwa jamii ya Wamasai ilikuwa ikiishi ndani ya maeneo haya ya uhifadhi pasipo utaratibu maalumu na mwongozo jamii hii ilikuwa katika janga kubwa la wanyamapori kama vile magonjwa maambukizo ya wanyamapori na majanga mengineyo.

Hivyo basi serikali ya wakoloni Waingereza wakati wa kipindi hicho iliamua kuanzisha maeneo mawili tofauti ya uhifadhi eneo moja la uhifadhi litumike maalum kwaajili ya uhifadhi wanyamapori pekee ambayo ndio Serengeti ya leo hii na vile vile eneo jingine la uhifadhi llitumike kama Hifadhi mseto ambapo Wamasai wataishi kwa pamoja yaani (Conservation). Hatimaye wamasai wote waliokuwa wakiishi Serengeti ya wakati wa kipindi kile wakahamishiwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ya leo hii.

Vilevile malengo mengine yalikuwa ni katika kulinda maslahi ya jamii ya kabila la wamasai ambao wameishi na wanyamapori pasipo uharibifu wowote ule kwa miaka na wanachukuliwa kuwa ni wahifadhi asili kwa sababu ya kuishi na wanyamapori kwa muda mrefu kihistoria.
Hata hivyo jamii ya Wamasai imeendelea kukua na kuwa na mifugo mingi hali ambayo kadiri tunavyoendelea kuishi mifungo inazidi kuwa mingi, hivyo kuhatarisha uwepo wa hifadhi hii miaka kumi ijayo kwa sababu wanyamapori watamezwa na mifugo ya wamasai.

Ipo haja ya serikali kuandaa utaratibu wa kuwahamisha Wamasai katika hifadhi hii ambayo kwa mujibu wa ilani ya CCM, inatakiwa iingizie pato la taifa la shilingi bilioni 6 ifikapo mwaka 2025.
Bila kufanya utaratibu wa kupunguza jamii ya wamasasi kwa kuwapa elimu ili nao wajue adhari za kuendelea kuzaana katika hifadhi hii; itakuwa kazi bure.
Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Dk Fredy Manongi alithibitisha kwamba ongezeko la binadamu ni kubwa hifadhini humo alipozungumza na wahariri na waandishi wa waandamizi wa habari wiki iliyopita.
![]()
“Kwa sasa hali ni ngumu kwa uhifadhi kwa kuwa kila hatua inayochukuliwa kwa ajili ya uhifadhi ina athari kwa wananchi wanaoishi ndani ya eneo hilo na kila shughuli za kibinadamu zinazofanyika zina athari kwa uhifadhi, na kwamba idadi ya watu imeongezeka kutoka 8,000 mwaka 1959 hadi 100,000 kwa sasa,” alisema.
Bahati nzuri niliwaona baadhi ya Wamasasi waliopewa elimu wakiwa wamenzisha maisha yao katika mji mdogo wa Mto wa Mbu kwa hiari yao na wengine wameajiriwa na kuwa madereva. Pongezi kwa viongozi wa hifadhi ya Ngorongoro kwa elimu hiyo ya kuwabadilisha wamasai hao kimawazo.
Hifadhi ya Mmlaka ya Ngorongoro ina ukubwa wa eneo lenye kilomita za mraba 8300 katika ukubwa wa jumla eneo lote na watu zaidi ya 200,000.

VIVUTIO VIKUU VYA UTALII HIFADHINI:
Eneo hilo linajumuisha Bonde la Ngorongoro (Ngorongoro Crater), Engaruka, Selela, Engaresero, bonde la Empakai, mlima Oldoinyo Lengai mlima pekee Tanzania ambao volkani yake bado ni hai, Bonde la Oldupai (Oldivai) sehemu ambayo ni chimbuko la historia ya binadamu.
Vilevile kuna misitu yenye madhari nzuri yenye kupendeza. Kwa mujibu wa maofisa wa hifadhi hii; Hifadhi inafikika wakati wote wa mwaka hasa mwezi Desemba, mpaka Februari, vilevile Mei mpaka Julai.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ipo karibu sana na mji wa Karatu kwa upande wa kusini ambapo hupatikana huduma za malazi na vyakula.
MAMBO YA KUFAHAMU:
Kama mtatumia usafiri wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuteremka katika bonde la Mgorongoro basi kuna ulazima wa kuwepo mawasiliano kuweza kufahamu kama huduma hiyo ipo au haipo kama huduma hiyo haipo basi utaratibu mwingine huandaliwa.
Kufahamu hayo yote ni lazima kuwasiliana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kama kuna uwezakano huo. Kampuni nyingi za binafsi hutoa huduma za kukufanikishia wewe kusafiri toka ulipo hadi bondeni Ngorongoro.
Tunahimiza utalii wa ndani kwani bei ya kutalii kwa mtanzania ni ndogo sana. Haizidi shilingi elfu 11 kwa mtu mzima na utakayoyaona ndani ya hifadhi ya Ngorongoro, utainjoi na utafurahia maisha. Anza leo kupanga kwenda kwenye hifadhi hii.