
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameonyesha kukerwa na na kile alichokisema Spika wa Bunge, Job Ndugai kuhusu Serikali kukopakopa badala ya kujiendesha kwa pesa za ndani.
Samia amesema hayo leo Jumanne, Januari 4, 2022 wakati akipokea ripoti ya matumizi ya Fedha za Maendeleo (Fedha za Uviko-19), Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Huwezi kufikiria mtu mliyemuamini, mshika mhimili, aende akasimame aseme yale. Ni stress ya 2025. Inashangaza kuona mtu mwenye uelewa, anasema kuna fedha ya tozo lakini kaenda kukopa, ya nini? Au kwa nini tunaendelea kutoa tozo wakati fedha ya mkopo ipo. Mawaziri tupeni hizo takwimu sasa hivi.
“Atakayekusumbua kwenye kazi yako, na uongozi wako ni shati ya kijani mwenzio wala si mpinzani. Mpinzani atakutazama unafanya nini, ukimaliza hoja zao hawana maneno. Lakini shati ya kijani mwenzio anayetizama mbele 2025/2030 ndiye atakusumbua.
“Nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu kutumia kila fursa nitakayoiona itakayoletwa ambayo naweza kuitumia kuleta maendeleo Tanzania nitaitumia. Sifanyi kwa ajili ya [uchaguzi wa] 2025, nafanya nimeapa kuleta maendeleo kwa Watanzania.
“Wakati mmenikabidhi huu mzigo, nilianza kusikia lugha zinasema serikali ya mpito, serikali ya mpito bungeni huko kwa kina Kassim. Nikarudi kwenye Katiba kuangalia serikali ya mpito imeandikwa wapi…sikuona. Nikasema ‘anhaa, twendeni.
“Nawashukuru wenyeviti wa CCM kwa kusimama na kutetea mkopo ulioleta maendeleo kwenu. Walipotokea wakuhoji mlisimama mkajibu, mkijua kwamba kinachofanyika ni utekelezaji wa ilani. Sasa mna mambo ya kwenda kifua mbele kwa wananchi kuwaambia CCM imefanya.
“Wakatizama mtu aliyeshika kitabu kuapa, wakamfanyia tathmini, wakamfanyia yote waliyoyafanya wakampa ‘grade’ yake wakamuweka pale. Sasa yanayotokea hawaamini, kwamba yule mtu waliyempa ile thamani ndio anayafanya. Hawaamini.
“Nataka niwaambie nitatoa list mpya [ya mawaziri] karibuni. Wale ninaohisi wanaweza kwenda na mimi…nitakwenda nao. Lakini wale wote ninaohisi ndoto zao ni kule, na wanafanya kazi kwa ajili ya kule, nitawapa nafasi waende wakajitayarishe vizuri huko nje.
“Hizi Fedha zitalipwa na wananchi kupitia tozo lakini wananchi wanatakiwa kuona matunda yake. “Na kwa maana hiyo ile hamu yao na tamanio lao la 2025 ‘somehow’ tamaa zinaondoka,” amesema Rais Samia.