
ZIKIWA zimesalia saa kadhaa kwa mwaka 2021 kupinduka na kuingia Mwaka Mpya wa 2022, miongoni mwa mastaa wakubwa wanaomaliza mwaka na kuingia mwaka mpya na kinyongo ni pamoja na Rajab Abdul au Harmonize na Raymond Mwakyusa au Rayvanny.
Mbali na Harmonize na Rayvanny, wasanii mbalimbali kwa mwaka 2021 walijikuta kwenye migogoro kutokana na sababu mbalimbali ambapo hadi mwaka unapinduka, bado ugomvi haujaisha.
HARMONIZE NA RAYVANNY
Tatizo la wawili hao lilikuwa wazi zaidi mwezi Aprili, 2021 baada ya Rayvanny kulalamika kuwa Harmonize alikwenda kwenye vyombo vya sheria kwa ajili ya kumshtaki kutokana na kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Paula Kajala; mtoto wa mwigizaji Kajala Masanja.
Vita hiyo ilizidi kupamba moto baada ya Harmonize kuachia Ngoma ya Vibaya ikizungumzia ishu hiyo kisha Rayvanny akajibu kwa Ngoma ya Nyamaza kabla Ibraah kumtetea Harmonize na wimbo wake wa Hayakuhusu. Hadi mwaka unapinduka bado hali si shwari kati yao.
SHILOLE NA KIBA
Tatizo la wawili hao lilibuka baada ya King Kiba kusema kwenye chombo kimoja cha habari kuwa hakumualika Shilole kwenye sherehe yake ya kusikiliza albam yake ya Only One King.
Kitendo hicho kilimuudhi Shilole ambaye alionesha dhahiri ni kwa jinsi gani alikwazika na kauli hiyo ya na kusema kuwa bado hawajakaa chini na Kiba ili kuzungumza.
HARMONIZE NA DULLY SYKES
Mgogoro huu uliibuka baada ya Dully Sykes kukubali kuwa yupo kwenye mchakato wa kumshtaki Harmonize baada ya kumtuhumu kutumia vionjo vya wimbo wake wa Bongo Fleva kwenye Amapiano yake ya Teacher.
SHILOLE NA SNURA
Wengine wanaoaga mwaka 2021 na kuingia 2022 wakiwa na kinyongo ni Shilole na Snura ambao ugomvi wao ni wa siku nyingi, lakini uliibuka upya 2021.
Snura ndiye aliyeingilia ugomvi wa Shilole na Kiba kwa kumtungia wimbo wa kumpaka uliokwenda kwa jina la Umealikwa ambao wasikilizaji walipigia mstari kwamba alimuimba mwenzake huyo.
AMBER LULU NA NAI
Hawa ni ma-video vixen na wasanii wa Bongo Fleva ambao kwa muda mrefu wamekuwa kwenye bifu huku chanzo kikisemekana ni mambo ya wanaume.
Hata hivyo, bifu hilo liliwaka zaidi 2021 baada ya kila mmoja kujitokeza hadharani na kumkandia mwenzake.
STORI; KHADIJA BAKARI, DAR