
Tukio lisilo la kawaida limetokea katika Kitongoji cha Kipondoda, Wilaya ya Manyoni mkoani Singida baada ya kaburi la mtoto Christina Samson mwenye umri wa mwaka mmoja, kufukuliwa kisha mwili wake kuchukuliwa na watu wasiojulikana.
Mtoto Christina alizikwa Jumapili ya Januari 16, mwaka huu ambapo ndugu zake walikuja kushtuka baada ya kukuta kaburi likiwa limefukuliwa huku jeneza likiwa tupu.
Juhudi za kuupata mwili wa mtoto huyo, bado zinaendelea huku simanzi kubwa ikiwa imetanda kwa ndugu na jamaa wa wamarehemu.
Inaelezwa kwamba matukio ya aina hiyo siyo mara ya kwanza kutokea wilayani Manyoni lakini safari hii imekuwa tofauti kwani mwili haujapatikana kabisa licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na ndugu wa marehemu.
Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwagisa amesema jeshi la polisi linaendelea kufuatilia tukio hilo ili kuwabaini watu wote waliohusika na kueleza kuwa wananchi wanapaswa kuelekeza nguvu zao kwenye maombi kwani vitendo hivyo vinaonekana kushamiri wilayani humo.