
Sakata la maiti kuopolewa katika Mto Yala nchini Kenya limechukua sura mpya baada ya maiti nyingine mbili kuopolewa hapo jana na kufanya jumla ya maiti 23 mpaka sasa ziopolewe kutoka kwenye mto huo.
Kamanda wa Polisi wa kaunti Ndogo ya Gem, Charles Chacha ameeleza kwamba baada ya miili hiyo kuopolewa kutoka kwenye mto huo, imepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Yala huku uchunguzi zaidi ukiendelea.
Tayari maiti hizo zimetambuliwa na ndugu zao ambao wanalalamika kwamba ofisi ya upelelezi wa makosa ya jinai, unawakatalia ndugu kuchukua miili hiyo kwa ajili ya mazishi kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi.
Wakizungumza kutokea katika hospitali hiyo, ndugu wa marehemu wamelalamika kwamba wamekataliwa kuchukua miili ya wapendwa wao mpaka vipimo vya vinasaba vitakapofanyika ili kujiridhisha kama waliojitokeza ni ndugu halisi wa marehemu hao, jambo ambalo wamedai linachelewesha shughuli za mazishi wakati tayari miili imeharibika.
Mutiso Nzomo ambaye ni ndugu wa Peter Mutuku ambaye mwili wake umeopolewa kutoka kwenye mto huo, amelalamika kwamba wamesafiri kutoka mbali katika maeneo ya Machakos na Kericho kwa ajili ya kuitambua miili hiyo lakini wanashangazwa na urasimu unaowekwa na jeshi la polisi nchini humo.
Malalamiko hayo yamewaibua watetezi wa haki za binadamu kutoka Shirika la Haki Africa ambapo wakurugenzi wake, Khalid Hussein na Boniface Mwangi wameitaka serikali kuwaruhusu ndugu waliowatambua wapendwa wao, kukabidhiwa miili kwa ajili ya mazishi badala ya kuendelea kuwazungusha.