
Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita katika visiwa vya Zanzibar alizaliwa mwanamke ambaye leo ni Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. Team Clouds imetua kule Unguja alipozaliwa.
Dada Mkubwa wa Rais Samia Suluhu Hassan anayefahamika kama Bi. Mgeni ambaye akiwa na miaka Saba alianza ukaishi naye kama mlezi wake.
“Alikuwa mtu mkimya sana kutokana na malezi aliyokuwa akilelewa tangu mwanzo. Nilimchukua akiwa na umri wa miaka Saba alikuwa akiishi na baba na mama yangu.
“Nilikuwa nafanya kazi hospitali nikapewa uhamisho kwenda Jambiani. Kule nilipewa nyumba na kituo changu. Alikuwa akisoma Skuli ya Raha Leo alipomaliza Raha Leo ndio akaenda kusoma Lumumba hadi alipomaliza shule.
“Rais Samia hajawahi kuja hapa kwangu na kunilalamikia kwamba kuna mtu anamkwaza au kuna kitu kinamkwaza hapana. Hajaniambia bado.
“Yeye ni mpenzi wa muziki wa Taarab, zamani alikuwa akija hapa akiwa na ndugu zake wanaweka muziki wa taarab wanacheza lakini sasa hivi tumeshakuwa watu wazima sio sana kusikiliza muziki huu hapa nyumbani kama zamani.
“Ni mchapakazi sana tangu akiwa mdogo hakuwa mtu wa kubweteka alipenda kupika, na kufanya kazi za nyumbani hakupenda kukaa tu afanyiwe kazi ndio maana hadi sasa akiwa kama Mkuu wa nchi anaendelea kuchapa kazi.
“Kwa sasa hivi akifika hapa nyumbani akitaka kufanya chochote watoto wanakataa wanamsaidia kazi. Na sasa hivi watoto wako wengi na pia kuna wajukuuu na watoto Wakubwa inakuwa sio vizuri kumwachia afanye kazi.
“Marafiki zake ambao alikuwa nao pamoja enzi za usichana wake hadi leo bado wapo na wakionana wanamwita Samia sio Mh. Rais kwa sababu wamezoeana sana.
“Alivyokuwa akikuwa mkubwa kiuongozi hatukuwa na wasiwasi kwa sababu tunajua ndio maendeleo hata alivyokuwa akienda kusoma hatukuwa na wasiwasi kwa sababu tulikuwa tunajua anakwenda kufanya la maana na alikuwa akimaliza anarudi,” Bi. Mgeni, Dada Mkubwa wa Rais Samia Suluhu Hassan