
OMARY Kivunja Ndamba siyo jina geni sana kwa wakazi wa mitaa ya Chang’ombe Unubini B Temeke Dar es Salaam, yeye ni mmoja kati ya wasomaji wakubwa wa magazeti bora ya michezo nchini ya Championi na Spoti Extra.
Lakini kama umeshindwa kupaelewa mitaa ya Chang’ombe Unubini B basi ni ile mitaa ya karibu na kiwanda kikubwa cha Serengeti, yaani ukifika mitaa hiyo ukamuulizia Mzee Ndamba basi utapelekwa hadi kwake hata na mtoto mdogo.

Mzee Ndamba mwenye umri wa miaka 64 ambaye ana tatizo la ulemavu wa miguu, lakini hilo halijakwamisha kufuatilia magazeti ya Championi na Spoti Xtra huku akiwa anahifadhi kwa miaka kadhaa kwa kila anaponunua magazeti hayo.
Licha kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa Simba lakini kwake haijawa kikwazo kusoma magezeti ya Championi na Spoti Xtra hata ambapo Yanga wanapokuwa moto, ambapo amekiri mwenyewe kuwa yeye ni mdau mkubwa wa makala ambazo zinaandikwa na wachambuzi mahiri wa magazeti hayo.
Championi limemtembelea mzee huyo nyumbani kwake mitaa ya Chang’ombe Unubini B, ambapo imeweza kushuhudia rundo la magazeti ambayo yamehifadhiwa na mzee huyo kila anaponunua kwa ajili ya kujisomea.

Mwandishi wa makala haya akiwa na Ofisa wa Masoko wa Global Publishers, Francis Johannes, wameweza kushuhudia magazeti ya kuanzia mwaka 2018, 2019, 2020, 2021 na sasa mwaka 2022 akiendelea kuyahifadhi.
Mzee Ndamba anasema yeye kwa sasa amejiajiri mwenyewe katika ofisi yake ndogo ya kutengeneza viatu vipya baada ya kutoka kwenye ajira yake ya awali, ambapo kazi yake kubwa ni kutengeneza na siyo kurekebisha kama wanavyofanya wengine.
Mzee huyo anasema kuwa: “Kwanza kifupi mimi ni fundi wa viatu yaani natengeza mwenyewe viatu kwa kufuata hatua zote, nimefungua ofisi yangu ndiyo ninapofanyia kazi siku zote na siyo mbali kutoka hapa nyumbani kwangu.
WEWE NI MWANACHAMA AU SHABIKI WA SIMBA?
“Nipo Simba miaka mingi sana lakini bado ni shabiki, sijawa mwanachama kwa kuwa sijaomba, nipo tangu mwaka 1970 ndiyo nilianza kuifuatilia.
“Suala la Uanachama kwangu siyo shida ila shida inakuja pale katika mlolongo wake kuwa na vikwazo vingi, ndiyo ambalo limekuwa likinichelewesha.
MAGAZETI HAYA UMEKUWA UKIHIFADHI KWA MIAKA MINGAPI?
“Kwanza hayo unayoyaona hapo ni magezeti ya Championi na Spoti Xtra ndiyo ambayo ninayasoma siku zote na suala la miaka mingapi nadhani inafika mitano kwa sababu yapo ya 2018, 2019, 2020, 2021 na 2022 japokuwa mengine ya zamani kuna wakati niliuza kwa wauza vitafunwa.
KITU GANI AMBACHO KIMEVUTIA KUSOMA CHAMPIONI NA SPOTI XTRA?
“Nadhani kitu kikubwa ni waandishi wake hasa upande wa uchambuzi wamekuwa wakiandika ukweli, angalia mtu kama Saleh Ally yeye anaandika uchambuzi au hata akitoa maoni basi huwa anasema ukweli bila ya kuangalia ni nani ambaye anamwambia.
“Kiuhalisia hayo mambo hayo ndiyo yamenifanya niwe msomaji mkubwa wa haya magazeti haya na wala siyo kuangalia nini kimeandikwa kwenye kurasa za mbele, maana wapo ambao wamekuwa wakifuatilia habari kwa kuangalia vichwa vya habari ila kwangu ni jambo la tofauti kabisa.
“Lakini kitu kingine ambacho kinapelekea haya magazeti ya Championi na Spoti Xtra yasinipite ni hadithi za Eric Shigongo.
HUWA UNAENDA UWANJANI KUIANGALIA SIMBA?
“Niliacha kwenda uwanjani mwaka 2008, nilikua mhudhuliaji mkubwa ila changamoto kubwa ni namna ambavyo miundombinu kwa watu wa aina yangu jinsi ilivyo.
“Ukiangalia kwa Uwanja wa Uhuru wakati ule watu wa aina yetu tulikuwa tunawekwa nyuma ya senyenge na unakuta wanakuja watu ambao wana afya bora zaidi yetu na kukaa kwenye yale maeneo na sisi kushindwa kuangalia kwa uzuri, ndiyo nilipoamua kubakia nyumbani na kuangalia kupitia runinga,” anasema mzee Ndamba.
Stori: Ibrahim Mussa, Dar es Salaam