
LICHA ya kushindwa kupata nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza cha Simba, beki wa kushoto wa timu hiyo, Gadiel Michael, amesema kuwa hana presha kwani itafika wakati wake wa kucheza.
Gadiel amekuwa akishindwa kupata nafasi ya kuanza mara kwa mara ndani ya Simba kutokana na uwepo wa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye wanacheza wote katika eneo la beki wa kushoto.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Gadiel alisema kuwa licha ya kushindwa kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza kwenye michezo ya ligi kuu, lakini anaamini kuwa wakati wake wa kucheza upo, hivyo hana presha ya kusugua benchi ndani ya kikosi hicho.
“Sina presha kwa kuwa sipati nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza kwani michezo ipo mingi ya kutosha na naamini kuwa nitapata nafasi ya kucheza huko mbeleni.
“Kila kitu ni mipango ya mwalimu hivyo nikipata nafasi ya kucheza huwa nashukuru lakini nikikosa nafasi ya kuanza basi huwa naamini kuwa itapatikana nafasi nyingine,” alisema beki huyo.
Joel Thomas, Dar es Salaam