
WANADAMU tumezoea ile tabia ya kumwaga sifa kemkem kwa mtu aliyetangulia mbele za haki lakini nami leo naomba nieleze ukweli kuhusu Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani uliopo Kata ya Kipunguni Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, ambaye ni Daniel Malagashimba kutokana na utendaji wake.
Tumezoea kuwaona wanasiasa wakiamka na kujifanya wako moto inapokaribia vipindi vya uchaguzi au wakati wa kampeni wakihofia kupoteza nafasi zao lakini hilo si kwa Malagashimba.
Ijumaa iliyopita nilikaribishwa katika mjadala wa maendeleo na kupinga ukatili wa kijinsia ulioandaliwa na Kituo cha Taarifa na Maarifa, Sauti ya Jamii Kipunguni kilichopo chini ya Mtandao wa Jinsia Nchini TGNP.

Katika mjadala huo watoto na wanafunzi nao walikaribishwa Malagashimba alichangia mambo kadhaa na alionekana kukemea sana unyanyasaji wa watoto, ndoa za utotoni na tabia ya ukeketaji.
Hata hivyo wakazi wengi wa eneo hilo wamesema tabia hiyo awali ilikithiri kwenye maeneo hayo lakini sasa imeanza kupungua kutokana na elimu inayoendelea kutolewa na viongozi wa mitaa.
Malagashimba aliwaambia watoto na watu walizima waliokuwa kwenye mkutano huo mtu yeyote awe mama, baba mtoto au yeyote anapoona anafanyiwa unyanyasaji wowote ule asiogope, afike ofisini kwake na kumueleza changamoto hiyo ili aimalize kwenye mtaa wake.

Mkutano huo ukielekea ukingoni lilikuja gari lililobeba maboksi ya madaftari ambayo yalianza kugawiwa kwa watoto waliokuwa kwenye mkutano huo na wazazi nao waliwabebea watoto zao ambao hawakufika kwenye mkutano huo.
Nilijiuliza kuwa madaftari hayo yametoka wapi ambapo ikabidi nimfuate muandaaji wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa, Fatma Abdulrahman ambaye aliniambia madaftari hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Daniel Malagashimba.
Nilimpongeza kimoyomoyo kwa upendo wake aliokuwa akiendelea kuuonesha kwa wananchi wake.
Wakati mkutano huo ukiendelea Malagashimba aliaga na kuondoka na mijadala iliendelea kwenye mkutano huo.

Mkutano huo ukiwa umemalizika mimi na wanahabari wenzangu Yasmine Protace wa Nipashe na Sabato Kasika wa The Guardian tulianza safari ambapo tukiwa njiani tulimuona mtu mmoja akiwa juu ya katapila kama akielekezana jinsi ya kuifanya kiufasaha kazi hiyo na dereva aliyekuwa akiliendesha.
Yule mtu kumbe alikuwa ni Malagashimba na dereva wa hilo katapila walikuwa wakichonga barabara za mitaa na kutawanya vifusi huku wakifukia mashimbo yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Hapo ukweli mimi na hao wanahabari wenzangu tulianza kumjadili kiupana zaidi jamaa huyu ambaye tulishawahi kumsikia sifa za utendaji wake kwa wakazi wa maeneo hayo kuwa jamaa huwa hapati usingizi kabisa panapotokea changamoto kwenye mtaa wake. Huyo ndiye Malagashimba wa Mtaa wa Amani Kipunguni. MAKALA HAYA YAMEANDIKWA NA RICHARD BUKOS WA GLOBAL PUBLISHERS