×

Serikali Yahimiza Wananchi Kulipia Kwa Wakati Viwanja Vilivyopimwa

Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda ya Dar es Salaam Bw. Idrisa Kaera (kushoto)

Serikali imetoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kulipia kwa wakati gharama za maandalizi ya Hati za viwanja vyao vilivyopimwa ili kuondokana na migogoro ya Ardhi inayokwamisha juhudi za maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda ya Dar es Salaam Bw. Idrisa Kaera wakati wa zoezi la ugawaji wa Hati za viwanja lililofanyika katika kata ya Kivule wilaya ya Ilala na kusisitiza kuwa Serikali imefanya kazi kubwa ya kurasimisha viwanja kwa wananchi lakini bado mwitikio wao wa kulipia gharama za hati zao umekua siyo wa kuridhisha.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda ya Dar es Salaam Bw. Idrisa Kaera (kushoto)

Kamishina Kayera amesema kuwa zaidi ya viwanja Elfu 76,000 vimepimwa Hadi Sasa lakini wananchi walioomba Hati ni Elfu 16,520 pekee, hivyo ameendelea kuwasihi wananchi kuongeza Kasi ya ulipaji wa gharama kwa ajili ya viwanja vyao.

 

Kuhusu gharama za upatikanaji wa hati Kamishina amesema Serikali imesikia kilio Cha wananchi na kupunguza Zaidi malipo Kutoka asilimia 15 mwaka 2014 hadi kufikia 0.5 kwa Sasa kulingana na thamani ya kiwanja husika, na zoezi la upatikanaji wa hati za Viwanja kwa sasa ni rahisi zaidi ambapo mwananchi anaweza kupata hati yake ndani ya siku mbili baada ya kukamilisha malipo na taratibu zote za kiwanja husika.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wakifuatilia kilichokuwa kikiendelea.

Kayera pia ametoa rai kwa makampuni yanayojihusisha na upimaji na urasimishaji wa viwanja kwa wananchi kufanya kazi kwa weledi na uhakika ili wananchi wapate hati zao mapema kama ambavyo wizara ya Ardhi na Serikali zimeelekeza juu ya umilikishwaji wa Viwanja kwa wananchi.

 

Kamishina Kayera ambaye aliambatana na maafisa wengine kutoka Wizara Ya Ardhi, Nyumba Na Maendeleo Ya Makazi amesema zoezi hilo la ugawaji hati litakua endelevu na wataendelea kuzunguka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Leave a Comment