
BARAZA la Vyama vya siasa nchini kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia (TGNP) na WiLDAF Tanzania wameendesha mashauriano ya kuleta namna bora ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi na uongozi katika vyama vya siasa kama sehemu ya uhamasishaji na utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa kipengele cha 6.

Mashauriano hayo yamefanyika Ofisi za Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP) zilizopo Mabibo, Dar na kufunguliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi ambapo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa akiwemo Mwenyekiti wa UDP, John Momose Cheyo, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ally Khatib pamoja na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza.

Katika mashauri hayo, mkufunzi wa masuala ya kisiasa, Profesa Ruth Meena alitoa mafunzo ya utawala bora kwa wajumbe waliohudhuria mkutano huo ambapo nayo yalijadiliwa kwa pamoja na viongozi hao.

Wawezeshaji wengine waliotoa mafunzo kwenye mkutano huo ni pamoja na Deogratius Koyaga, Idd Mziray na Dkt. Avemaria Semakafu.

Baada ya kutolewa mapendekezo mbalimbali na viongozi hao, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa (Nyahoza) alisema anayachukua na kuyafikisha sehemu husika kwa ajili ya kuyafanyiwa kazi.

Malengo Mahsusi ya Mashauriano hayo ni:
1.Kukumbushana mapendekezo yaliyojitokeza na kuchagua mapendekezo ya kipaumbele yatakayopelekwa kwenye Baraza la Vyama vya Siasa kupitia ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ili kuingiza na kutekeleza masuala ya kijinsia, katika katiba, miongozo na ilani za vyama vya siasa.
2.Kufahamishana na kujadiliana kuhusu sera inayozingatia masuala ya kijinsia na mfumo wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi wa siasa.
3.Kutengeneza mwongozo wa sera inayozingatia masuala ya kijinsia katika vyama vya siasa na mfumo wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi wa siasa.
HABARI/PICHA NA RICHARD BUKOS /GPL