
MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA), kupitia Kitengo cha Stempu za Kielektroniki (ETS) imesema, kampeni yake ya HAKIKI STEMPU ngoma yake haitalala mpaka kieleweke.
Afisa kutoka ETS, Elias Mashenene amesema hayo leo (Jumatatu) kwenye kipindi cha Front Page kinachorushwa laivu na +255Global Radio na Global TV Online alipokuwa akielimisha umma umuhimu wa kuhakiki ubora wa bidhaa kabla ya kuitumia.
“Tumeanza kuweka stempu zetu kwenye vinywaji baridi na vinywaji vikali kama Mvinyo pamoja na sigara,Hatua hii kwanza inamlinda mtumiaji wa bidhaa hizo, kwani anaweza kuskani stempu zetu na kubaini kama bidhaa anayotaka kutumia ni feki au ni halali lakini inadhibiti pia ukwepaji kodi,” alisema Mashenene.

Naye Merey Macha afisa mwingine kutoka ETS alisema, kampeni hii ambayo ni ya kudumu inaambatana na elimu kwa umma itakayomuwezesha mwananchi wa kawaida kujua ni njia zipi anaweza kuzitumia kuhakiki stempu za ETS.
“Kampeni hii inaambatana na elimu, tumejipanga kuhakikisha kuwa kila mwananchi anaelewa na kusema kweli hakuna ukomo katika jambo hili,” alisema Merey.

Timothy Mgaya afisa mwingine kutoka ETS alisema wakati wanaendelea na zoezi hili timu ya wataalam wao inaendelea kufanyia kazi changamoto zote na kuzipatia ufumbuzi.
Akijibu swali la mmoja wa watangazaji wa kipindi hicho, Happyness Gidion aliyetaka kujua ni hatua gani zinaweza kuchukuliwa kwa mtu ambaye anakwepa kupandika stempu za ETS au kuweka feki, Mashenene alisema:
Sheria zipo wazi, mtu huyo akikamatwa anaweza kufungwa, kupigwa faini au vyote kwa pamoja.
Stori: Richard Manyota