
MARA baada ya kutua jijini Casablanca, Morocco, wachezaji wa Simba wamelalamikia hali ya hewa ya baridi kali lililopo nchini humo.
Simba inatarajiwa kucheza mchezo wake wa tatu wa Kombe la Shirikisho Afrika keshokutwa Jumapili saa 4:00 Usiku kwa saa za Tanzania, kwenye Uwanja wa El Massira uliopo Berkane
. Akizungumza na Championi Ijumaa, beki na kiungo mkongwe wa timu hiyo, Erasto Nyoni alisema kuwa mara baada ya kutua Morocco wamekutana na sapraizi ya hali ya hewa ya baridi kali.
Nyoni alisema kuwa hali ya hewa hiyo waliitarajia baada ya kupata taarifa kwa baadhi ya viongozi waliotangulia Morocco kwa ajili ya kuandaa mazingira ya timu.

Aliongeza kuwa, hali ya hewa hiyo haitawafanya wao wapoteze mchezo huo na badala yake watapambana uwanjani na hatimaye kupata matokeo mazuri ya ushindi yatakayowawezesha kuongeza idadi ya pointi katika kundi lao.
“Tumetoka Niger kucheza na Gendarmarie ambako huko tulikutana na hali ya hewa nzito ya joto kali, tumefika hapa tumekutana na sapraizi ya baridi kali.
“Hiyo ni moja ya changamoto kubwa tuliyokutana nayo hapa Morocco, lakini kama wachezaji tutajitahidi kupambana na hali ya hewa hii tuliyokuta hapa Morocco.
“Tuwapongeze viongozi kwa kutuwahisha kufika hapa Morocco, hiyo itatusaidia kuzoea hali ya hewa hapa kwa siku hizi tano tutakazokaa kwa maana ya leo Jumatano hadi Jumapili siku ya mchezo huu,” alisema Nyoni.
Wilbert Molandi na Musa Mateja