
BAADHI ya barabara ndani ya manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, zinatarajiwa kufungwa ili kutoa nafasi kwa washiriki wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2022 kushirika vyema na kwa usalama.
Hayo yako kwenye taarifa iliyotolewa mjini Moshi leo na waandaji wa mashindano hayo, ambapo kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi huo unalenga kuhakikisha usalama wa washiriki wote.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kufungwa kwa baadhi ya barabara hizo ni kutokana na ukweli kwamba washiriki watatumia barabara hizo ikiwemo barabara kuu na kwamba madereva watatakiwa kutumia njia mbadala zilizoko maeneo mengine katika manispaa hiyo na pembezoni mwake ili kuepusha usumbufu kwa wakimbiaji.
Katika ufafanuzi wake, taarifa hiyo imeeleza kuwa magari yatakayotokea Jiji la Arusha itabidi yasimamishwe kwa muda katika maeneo ya mzunguko wa Arusha na ule ulio eneo la YMCA kwa muda mfupi ili kupisha wakimbiaji kuvuka barabara katika maeneo hayo.
Hatua hii pia itawaathiri madereva wa magari kutoka Dar es Salaam, Marangu na Himo, ambapo washiriki wa mbio hizo wanapaswa kuwa wameondoka kwenye barabara hizo ifikapo saa 3 asubuhi.
Kwa yale yanayotokea eneo la Machame wilaya ya Hai hadi Barabara ya Sokoine, barabara hiyo itafungwa katika eneo la barabara ya Shanty Town majira ya saa 12 asubuhi sambamba na ile ya mchepuko kwenye Barabara ya Lema.
Barabara ya kutoka Rau hadi Moshi Mjini, itafungwa kuanzia saa 1 hadi saa 3 asubuhi ili kutoa nafasi kwa ajili ya mbio za kujifurahisha za kilomita 5 (Fun Run 5Km).
“Barabara kati ya Masoka hadi Mweka pia itafungwa kati ya saa 1 hadi saa 3 asubuhi”, ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Waandaaji hao pia walitangaza maeneo mawili ya kukaa washiriki wa mbio hizo ambayo walisema ni pamoja na eneo la Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) upande wa Mashariki, eneo ambalo kufikika kwa urahisi kwa kupitia Barabara ya Uru hadi katika viwanja vya MoCU na pia katika viwanja vya Shule ya Polisi Moshi vinavyoweza kufikiwa kwa kupitia barabra ya Kilimanjaro.
“Mengi ya maeneo haya yana nafasi nyingi na maandalizi yanayolenga kuyatayarisha kwa ajili ya shughuli hiyo yanakaribia kumalizika”, ilisema taarifa hiyo, ambapo pia taarifa hiyo iliwataka waaashiriki wote kuwa waangalifu wanapokuwa barabarani ili kuepuka ajali.
Aidha taarifa hiyo imeeleza ya kuwa kutakuwa na maeneo mawili ya kuegesha magari, yakiwemo magari madogo na mabasi.
Kwa wale wanaotumia mabasi madogo/teksi kushuka watakuwa katika sehemu mbili za maegesho au kando ya barabara.
“Hakutakuwa na njia ya kuingia MoCU kutoka Barabara ya Sokoine kuanzia saa 12 asubuhi, hivyo wale wote ambao watakuwa na nia ya kuitumia barabara watalazimika kushuka kwenye kona kati ya barabara ya Sokoine na ile ya Kilimanjaro.
Wadhamini wa mashindano haya ambayo yanaingia mwaka wake wa 20 tangu kuanzishwa kwake ni pamoja na Kilimanjaro Premium Lager- Mdhamini Mkuu, Tigo-21km, Grand Malt -5km.
Wadhamini wa meza za maji ni pamoja Absa Tanzania, Unilever Tanzania, TPC Sugar, Simba Cement, Kilimanjaro Water; wafadhili wengine ni pamoja na GardaWorld Security, Keys Hotel, Kibo Palace Hotel, Surveyed Plots Company Ltd, Bodi ya Utalii Tanzania na CMC Automobiles.
Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zitanazotarajiwa kufanyika Jumapili Februari 27, 2022 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), zimeandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa hapa nchini na kampuni ya Executive Solutions Limited.