×

Sugu: Sina Waganga Kwangu Mungu Ndiye Muumba

 

MIAKA kadhaa iliyopita, ilikuwa kama msiba pale ziliposikika tetesi za aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mijini, Joseph Mbilinyi almaarufu Sugu au Mr II kwamba ataendelea kujikita kwenye siasa na huwenda akaachana kabisa na muziki.

 

Ikumbukwe kwamba, kabla ya kuwa mbunge kwa miaka kumi tangu 2010 hadi 2020 nafasi yake ilipochukuliwa na Spika Dk Tulia Ackson, Sugu ni mmoja wa waasisi wa muziki wa Kizazi Kipya nchini Tanzania akijikita kwenye mahadhi ya kufokafoka (Hip Hop) tangu miaka ya 1990.

 

Sugu ana historia yake; ni msanii wa kwanza kurekodi albam ya miondoko ya Hip Hop ya Kiswahili kwa gharama ya juu zaidi ndani ya Studio za MJ Records chini Master Jay.

 

Ni miongoni mwa waanzilishi wa awali kabisa wa Hip Hop Bongo akiwa na Da Young Mob ambao alishirikiana nao katika kinyang’anyiro cha Yo Rap Bonanza lililokuwa linaandaliwa na akina Kim The Boyz na Ibony Moalim katika miaka ya 1990, kabla ya kuwa rapa wa kujitegemea na kutoa albam yake ya kwanza iliyokwenda kwa jina la Ni Mimi mwaka 1995.

 

Mbali na kuwa rapa, Sugu ni mwanaharakati wa haki za binadamu, mwanasiasa na mfanyabiashara.

 

Aina ya mashabiki wa Sugu siyo hawa wa kizazi cha kina Diamond Platnumz na Harmonize; ni wale wa kizazi cha Profesa Jay, Lady Jaydee, AY, Juma Nature, marehemu Mangwair na wengine wa enzi hizo.

 

Hao ndiyo waliohuzunika waliposikia Sugu anawaza kuachana na muziki ili afanye majukumu mengine, hasa ya kisiasa na kibiashara.

 

Wakati ule, hoja ya Sugu ilikuwa; “Kuliko kuwa kimya bila kuwa active kimuziki nadhani sasa nalazimika kufikia mwisho na soon nitaweka rasmi mic chini.

Umri nao unasonga na majukumu mengine yanayohitaji muda wangu zaidi yanaendelea kuongezeka kwa neema zake Mungu.”

 

Mara ya mwisho, Sugu aliachia Albam ya Veto mwaka 2009, lakini alikuwa akitoa ngoma kadhaa mojamoja kama Freedom kabla ya kutangaza rasmi uamuzi huo.

 

Hata hivyo, mashabiki wale waliomkosa Sugu kwa miaka kadhaa, sasa wanatabasamu baada ya kusikia ngoma yake mpya ya Taita akiwa na rapa wa kizazi cha sasa, Billnass au Nenga na muunganiko wao unatajwa kulipa ile mbaya kwa mashabiki wao Akizungumza na Gazeti la IJUMAA namna alivyofurahi kufanya kazi na Sugu, Nenga anasema;

“Nimekuwa shabiki mkubwa wa muziki wa Bongo Fleva kabla ya kuwa mwanamuziki, nimekuwa nikifuatilia na kusikiliza kazi za wasanii mbalimbali za waasisi ndizo zimenijenga mimi kuwa mwanamuziki kwa sababu nilianza kupenda na kukariri nyimbo za watu.

 

“Sugu ni moja kati ya wasanii ambao nawapenda na ninaheshimu mchango wao kwenye sanaa kwa sababu wasingekuwepo watu kama hao labda mimi nisingefanya hiki ninachokifanya. Huwa naheshimu kile alichokifanya napenda kazi zake na zipo nyingi zilizokuwa zikinibamba, ni kaka na nimekuwa nikisapoti vitu vyake vingi.”

 

Miongoni mwa vitu vilivyokuwa vikisubiriwa na urejeo wa mkongwe wa Sugu kwenye muziki.

Hata hivyo kuna jambo ambalo limekuwa gumzo mno kwenye ngoma hiyo; hili si lingine bali ni majibu aliyoyatoa Sugu kwenye sehemu ya mashairi ya ngoma hiyo.

Wakati f’lani Sugu, mwaka 2019, Sugu alimuoa binti aitwaye Happyness Msonga na ikumbukwe kwamba amezaa mtoto wa kike na mwanamama wa Bongo Movies, Faiza Ally aitwaye Sasha Joseph.

 

Ukweli ni kwamba kulikuwa na vita ya maneno kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya Happyness ikidaiwa mashambulizi hayo yaliongozwa waziwazi na Faiza ambaye hakuamini kumuona baba wa mtoto wake akimuoa mwanamke mwingine zaidi yake.

 

Hapo ndipo kulipoibuka madai mazito kwamba Sugu ameoa mwanamke ambaye ni mgumba, lakini kupitia wimbo huo wa Taita, mwamba huyo anawajibu wale walioeneza maneno hayo kwa kusema;

 

“Sina waganga kwangu Mungu ndio muumba, kumbuka wadangaji wa Insta waliposema wife wangu mgumba, hatukuwajibu, tukawajibu kwa mimba, leo tuna watoto wanagawana vyumba kwenye mjumba…” Akimaanisha hakuona sababu ya kuwajibu kwa maneno kwani wengine hutaka kujibizana, badala yake akawajibu kwa vitendo na sasa yeye na mkewe Happyness wamejaaliwa watoto wawili.

Leave a Comment