
Rais Samia Suluhu ametembelea Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa leo ambapo akiwa Shuleni hapo ametimiza ahadi ya kukutana na Mwanafunzi Emmanuel Mzina ambaye aliwahi kuongea nae kwenye simu na Mwanafunzi huyo akaomba kuonana na Rais.
Baada ya mazungumzo mafupi, Emmanuel aliomba apate nafasi ya kuzungumza mazungumzo ya faragha na Rais Samia na Rais akakubali ombi hilo.
“Nilipokuwa ndani kule mwanangu Emmanuel aliomba fursa ya kuongea nami, akasema nina ‘personal issue’ naomba wanipishe, na mimi nikaomba tupisheni niongee naye.
“Emmanuel ameniambia, namshukuru sana Mama yangu pamoja na changamoto alizonazo za maisha amejitahidi nimesoma mpaka kufikia hapa, mwaka huu nitafanya mtihani wa kidato cha sita, sina matumaini ya kupata ajira za serikali hivi nilivyo.
“Lakini nakuomba Mama nikimaliza kidato cha sita nisomeshe nje na la pili nifungulie taasisi yangu mwenyewe, lengo langu ni kuwasemea watoto kama mimi waliofichwa majumbani watolewe waje wapate elimu, hilo ndilo nililoongea na Emmanuel, pamoja na mawili matatu ambayo ni siri yetu, na mimi nikamuahidi nitafanya hivyo,” amesema Rais Samia.