×

Binti wa Umri wa Miaka 7 Afariki Ukraine

Watu sita akiwemo binti mwenye umri wa miaka 7, Alisa Hlans wamefariki dunia baada ya majeshi ya Urusi kurusha makombora katika shule moja katika Mji wa Okhtyrka huku babu wa binti huyo ambaye alijaribu kumuokoa mjukuu wake, naye akiuawa katika shambulio hilo.

 

Hapo jana, mke wa Rais wa Ukraine, Vodomyr Zelensky, Olena Zelenska, alitoa kauli kwamba kuna takribani watoto 37 waliouawa tangu majeshi ya Urusi yalipoivamia Ukraine na kuzitaka jumuiya za kimataifa kuingilia kati.

 

Picha za tukio hilo, zinaonesha miili ya watu kadhaa waliofariki dunia, ikiwa katika lango la kuingilia kwenye shule hiyo ambapo inaelezwa kwamba waliuawa wakati wakijaribu kukimbia baada ya majeshi ya Urusi kuanza kuishambulia shule hiyo.


Mwendesha mashtaka mkuu wa Ukraine, Irina Venediktova amenukuliwa akisema binti huyo aliyeuawa, alikuwa amebakiza miezi mitatu kutimiza umri wa miaka nane na kueleza kwamba Urusi ilitumia mabomu ya ‘cluster’ ambayo yamezuiwa kutumika duniani kote kutokana na madhara yake.

 

Urusi imekanusha kuishambulia shule hiyo wala kutumia mabomu yaliyokatazwa na kueleza kwamba habari za tukio hilo ni propaganda zinazoenezwa na Serikali ya Ukraine.

🔴#LIVE: RAIS SAMIA ANASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI – ZANZIBAR

Leave a Comment