
JESHI la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam kwa kus hirikiana na Kikosi Kazi cha Kuzuia na Kupambana na Ujangili limewakamata watu watatu wakiwa na vipande 25 vya meno ya tembo idadi inayoashiria kuwa tembo 14 wameuawa.
Vipande walivyokutwa navyo vina uzito wa kilogramu 20.9, vilikuwa vimefichwa ndani ya nyumba ya mmoja wa watuhumiwa hao kutokana na operesheni hiyo ya Polisi iliyo fanyika Ubungo NHC.
Waliokamatwa ni mkazi wa Ubungo, Gabriel Mgana na wenzake wawili ambao ni wakazi wa Kinyerezi wilayani Ilala, Haffarman Yona na Felician Cyril (57).
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro alibainisha kuwa gari lililotumika lilikuwa lenye namba za usajili T. 818 DCA aina ya Toyota Wills.
Alisema uchunguzi wa kina unafanywa kujua tembo waliouawa ni wa eneo lipi na thamani ya meno hayo ni kiasi gani na yalikuwa yanatarajiwa kupelekwa au kuuzwa wapi.
“Hili ni tukio baya na wale wote waliohusika watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali, kwa sasa jeshi linawashikilia hawa watatu, lakini mtandao mzima utakamatwa,” alisema Kamanda Muliro.
Aidha, alisema wanamshikilia mkazi wa Banana Kitunda, Khatib Abdalla na wenzake watatu kwa tuhuma za wizi kwa njia ya mtandao.
Alisema askari baada ya kumkamata Abdalla na kwenda kupekua nyumbani kwake, wa likutwa na laini 46 za mitandao ya simu tofauti tofauti, vizibao vinne vya uwakala, simu za mkononi 14 na vitambulisho vitatu vyenye majina feki.
Alisema wamekuwa wakitumia laini hizo kuwaibia watu mbalimbali wakijidai wanatoa huduma za kusajili laini za simu lakini wanaishia kuwaibia wateja wao.
Polisi pia wamekamata magari matatu yaliyoibwa Dar es Salaam kwa nyakati tofauti.
Kamanda aliyataja magari hayo yenye namba za usajili T. 347 DXG aina ya Nisan Extray na jingine lenye namba za usajili T. 317 DAN aina ya Passo na lenye namba T 707 DVH Toyota Prado ambayo yaliibwa.