
KUTOKANA na kukosekana kwa kiungo Mzambia, Clatous Chama katika michezo ya kimataifa kutokana na taratibu za kikanuni, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco ameamua kuwatumia mastaa Pape Sakho, Bernard Morrison na Rally Bwalya kwa ajili ya kubeba majukumu hayo.
Tangu arejee ndani ya kikosi cha Simba, Chama amefanikiwa kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Pablo, ambapo kocha huyo amekuwa akimtumia kama kitovu cha kutengeneza mabao kwa kufunga na kuasisti.
Chama ambaye anatumika kwenye ligi kuu na Kombe la Shirikisho la Azam, anazuiwa na kanuni za Shirikisho la Soka Africa (Caf), kuichezea Simba kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuwa tayari alishaichezea Berkane kwenye michuano hiyo.
Championi Jumamosi, ambalo lilihudhuria mazoezi ya Simba ya kujiandaa na mechi hiyo dhidi ya Berkane juzi Alhamisi, lilishuhudia kocha huyo katika vipindi tofauti akiwatumia Bwalya, Sakho na Morrison kucheza namba 10 anayocheza Chama kikosini hapo.
Akizungumzia kuhusu hilo kocha Pablo alisema: “Tunamkosa Chama, wote mnajua sababu ya hilo, lakini hatuna sababu ya kutetereka kwa kuwa tunao wachezaji bora ambao wanaweza kucheza eneo hilo na kuhakikisha tunapata matokeo.”
Stori: Joel Thomas