
LICHA ya Chico Ushindi kutoonesha kiwango kizuri hadi hivi sasa, lakini Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi, amempa kiungo huyo majukumu mapya ya kupiga kona zote.
Nyota huyo aliyesajiliwa na Yanga katika usajili wa dirisha dogo msimu huu, alianza kufanya majukumu hayo katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar.
Mkongomani huyo tangu atue Yanga akitokea TP Mazembe, bado hajaonesha kiwango bora kama ambavyo ilitarajiwa.
Chico katika mchezo dhidi ya KMC, alipiga kona tano, moja ikizaa bao lililofungwa na beki wa kulia, Djuma Shaban kwa kichwa.
Akizungumzia hilo, Nabi alisema: “Chico ndiye nimempa jukumu la kupiga mipira ya kona na faulo muda mwingine kila inapotokea kama Saido anakuwa hayupo.
“Katika mchezo huu dhidi ya KMC, Chico alikuwa anafahamu majukumu yake niliyompa ya kupiga mipira hiyo baada ya kumuona ana uwezo mkubwa.
“Nilimpa jukumu hilo baada ya kukosekana Saido kutokana na majeraha, nilikuwa nimemuandaa tangu mazoezini, nimpongeze alitimiza majukumu yake vizuri na kufanikiwa kutengeneza bao la pili,” alisema Nabi.
STORI: WILBERT MOLANDI