×

Korea Kaskazini Yafyatua Tena Kombora

KOREA Kaskazini imefanya majaribio ya kufyatua tena kombora la masafa marefu Alhamisi ya Machi 24, 2022 baharini na kufanya mpaka sasa iwe imefyatua makombora 12 tangu mwaka huu ulipoanza.

 

Afisa wa ngazi za juu wan chi jirani ya Korea Kusini, amesema bado hawajapata taarifa kamili kuhusu aina ya kombora lililofyatuliwa na kueleza kuwa taarifa za awali zinaonesha kwamba ni kombora la masafa marefu.

 

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Japan na Ofisi ya Waziri wa Ulinzi nchini humo, wamesema uwezekano mkubwa ni kwamba kombora hilo ni la masafa marefu linaloweza kusafiri kutoka bara moja hadi jingine (ICBM) na kueleza kwamba walinzi wa Pwani ya Japan, wametoa tahadhari kwa vyombo vinavyopita jirani na eneo yalipofanyika majaribio hayo.

 

Majaribio hayo yanakuja muda mfupi baada ya Jumapili iliyopita, Korea Kaskazini kufyatua tena kombora jingine ambapo licha ya malalamiko kutoka kwa jamii ya kimataifa zikiwemo nchi za Japan na Korea Kusini, Rais Kim Jong Un ameendelea na mfululizo wa majaribio hayo.

 

Baadhi ya watafiti wa siasa za Korea Kaskazini, wameonya kwamba huenda mfululizo wa majaribio ya silaha nzito yanayofanywa na Korea Kaskazini, ni salamu kwa Marekani ambayo uhusiano kati ya mataifa hayo, umeendelea kulegalega hususan kuhusu makubaliano ya silaha za nyuklia ambayo yamekuwa yakikwama mara kwa mara.

 

Katika siku za hivi karibuni, Korea imefanya majaribio ya silaha mpya na za kisasa zaidi, yakiwemo makombora ya hypersonic ambayo yanatajwa kuwa na uwezo wa kusafiri kutoka Korea Kaskazini mpaka nchini Marekani kupitia anga la bahari ya Pacific.

 

Pia imefanya majaribio ya makombora hatari ya makombora ya masafa marefu ya Hwasong-17 ambayo bado yanaendelea kuboreshwa ili yafike mbali zaidi.

 

Maafisa wa Korea Kaskazini, wamedai kwamba majaribio mapya, si kwa lengo la kumtisha yeyote bali yanatumika kupima na kuboresha kamera maalum za satellite zinazotumika kwenye masuala ya ulinzi ili kuilinda nchi hiyo na mashambulio ya anga.

Leave a Comment