×

Coastal: Tunaijua Mipango ya Simba Tumejipanga Kuibuka na Ushindi Uwanja wa Mkwakwani

Kikosi cha timu ya Simba.

UONGOZI wa Coastal Union umefunguka kuwa unafahamu vizuri mipango ya wapinzani wao, Simba na watafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa wanaiharibu na kuibuka na ushindi.

 

Coastal leo wanatarajia kuwa wenyeji wa Simba katika mchezo wa ligi utakaopigwa Uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Ofisa Habari wa Coastal Union, Jonathan Tito, alisema: “Kila kitu kipo kamili kuelekea mchezo huu, hatuna presha ya aina yoyote kwa sababu Simba ni timu ya kawaida kama zilivyo timu nyingine kwenye mashindano haya ya ligi kuu hivyo tuna uhakika kuwa tutapata ushindi wa pointi tatu.

 

“Tunazihitaji alama tatu zaidi kuliko mpinzani wetu ambaye anazihitaji alama hizo ili kumfikia mpinzani wake Yanga, sisi tunahitaji kutimiza malengo yetu kwa hiyo tuna sababu yenye maana zaidi kuliko wao za kupata ushindi kwenye mchezo huo.

 

“Sina cha kuwaambia Simba zaidi ni kuwa wasitegemee kwa vile walimfunga US Gendarmerie basi wataweza kutufunga na sisi, wakumbuke kuwa kwenye mzunguko wa kwanza tulicheza nao kwa Mkapa tena tukiwa pungufu na bado hawakuweza kupata ushindi mbele yetu.”

 

Coastal Union inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikifanikiwa kukusanya pointi 11 kwenye michezo 18 waliyoshuka dimbani.

Leave a Comment