×

HADITHI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 3


MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)
0719401968
ILIPOISHIA:
Nikiwa sielewi hili wala lile, nilimuona mmoja kati yao akirudi pale kwenye pikipiki, nikamuona akifungua kidumu kilichokuwa na kimiminika ndani yake ambacho kwa mbali sikuweza kugundua ni nini. Akarudi ndani kwa wenzake na kufumba na kufumbua, nilishtuka kuona moshi mwingi ukianza kutokea madirishani na pembeni ya paa.

SASA ENDELEA…
Wale watu wakatoka haraka nje, wakadandia pikipiki zao na kuziwasha, wakasogea mita kadhaa na kugeuka tena nyuma, nadhani ili kuhakikisha kama walichokusudia kukifanya kinaenda kama walivyokuwa wamepanga.

Nilishindwa kujizuia pale juu ya mti kutokwa machozi, baada ya kuona nyumba yetu kuukuu ikiteketea kwa moto huku wakigongesheana mikono kwa furaha na kuondoka kwa kasi kubwa na pikipiki zao.

Nilikuwa na uwezo wa kufanya kitu lakini niliona si busara kwa sababu naweza kujikuta naharibu zaidi mambo.

Basi niliendelea kushuhudia nyumba yetu ikiteketea huku moshi mkubwa ukiwa umetanda angani, na kwa jinsi moto ulivyokuwa mkali, sikuweza kuokoa chochote.

Nilishuka na kukaa nje, mita kadhaa kutoka moto ulipokuwa unawaka kwa nguvu, nikawa nimejishika tama huku moyoni nikiwa na uchungu usiomithilika.

Kwa ilivyoonesha, mtu aliyekuwa nyuma ya matukio yote hayo, alikuwa akitamani kuniona napata shida kubwa pengine kuliko binadamu yeyote aliyewahi kuishi.

Kilichonifikirisha zaidi, kama mtu au watu waliokuwa wanayafanya haya walikuwa na lengo la kuniua, kwa nini jana yake walipokuja hapo nyumbani na kumteka Saima, hawakunipiga risasi na kuniua kabisa wakati walikuwa na uwezo wa kufanya hivyo? Kwa nini waliniacha niendelee kuishi?

Kwa jinsi nyumba zilivyokuwa zimejengwa hapo kijijini kwetu, na kwa sababu sikupiga kelele zozote za kuomba msaada, wanakijiji walikuja kuanza kukusanyika wakati moto ukiwa unaelekea kuzimika baada ya kuwa umeteketeza kila kitu.

Kwa sababu ninazozijua mwenyewe, sikutaka kuzungumza na mtu yeyote, nikawahi kuondoka kabla hawajafika na kurudi kule vichakani.

Nilikuwa nahitaji muda wa kukaa peke yangu, kutafakari juu ya kilichotokea na kuchukua uamuzi wa nini cha kufanya.

Kwa hiyo niliendelea kujichimbia kule vichakani, machozi yakinitoka na kuulowanisha uso wangu, nikawa natafakari nini cha kufanya.

Nilikaa huko mpaka giza lilipoanza kuingia, nikavaa koti langu na kuhakikisha kama kitendea kazi changu kipo kwenye hali nzuri, nikaianza safari ya kuelekea mjini kwa sababu katika kutafakari, niliamua kwamba dawa ya tatizo siyo kulikimbia, ni kukabiliana nalo.

Kwa kuwa nilikuwa na picha ya watu waliokuja kuchoma ile nyumba yetu na nilikuwa nafahamu wapi kwa kuwapata, niliamua kuwafuata hukohuko ili kama ‘mbwai iwe mbwai.’

Huu ni uamuzi wa kijasiri sana ambao unahitaji kweli uwe na moyo wa kishujaa kuuchukua kwa sababu watu niliokuwa nawafuata hawakuwa wa mchezomchezo lakini ilikuwa ni lazima niende.

Niliamua kutembea kwa miguu kwa sababu kwa hali niliyokuwa nayo, kama ningeamua kupanda gari ingekuwa rahisi kwa watu kunishtukia kwamba nilikuwa na ‘chuma’ begani na pengine kunikamatisha kwa polisi.

Baada ya kutembea kwa muda mrefu, hatimaye niliwasili jijini Dar es Salaam na moja kwa moja nilienda Manzese Tip Top, kwenye maskani ya mmoja kati ya wale vijana aitwaye Ismail au Suma Baunsa kama tulivyozoea kumuita.

Suma alikuwa akiendesha biashara ya kuuza vinywaji kwenye grosari moja pale Manzese Tip Top na sifa kubwa ya grosari yake ilikuwa ni kuuza kila aina ya pombe unayoitaka, kwa saa ishirini na nne.

Kwa nje ungeweza kudhani kwamba ni nyumba ya mtu lakini kumbe ndani kulikuwa na ukumbi mkubwa ambako pombe zinauzwa usiku kucha na mchana kutwa.

Nilijua kwa vyovyote lazima Suma atakuwa kwenye ofisi yake akisherehekea na wenzake kwa sababu mara zote, hata kipindi ambacho tulikuwa tukishiriana nao kabla sijaamua kuachana na hayo mambo na kuendelea na maisha yangu, tulikuwa tukipiga ‘ishu’, tunakaa nao kwenye chimbo hilo kuwakwepa polisi.

Baada ya kufika eneo hilo, nilijua nikipitia mlango wa mbele, ni rahisi mabaunsa wake kunishtukia na pengine kunizuia kuingia, kwa hiyo kwa sababu nilikuwa nazijua njia za mkato za kuingilia ndani, nilitazama huku na kule na nilipojiridhisha kwamba hakuna aliyekuwa akinifuatilia, niliruka ukuta mrefu wa uani, nikatua ndani kimyakimya.

Nikaingia kwenye moja kati ya vyoo vya wanaume vilivyokuwa huko uani, nikaikoki bunduki yangu na kuikamata vizuri mkononi, nikatoka huku nikitembea kwa staili ya kuyumbayumba ili watu waamini nilikuwa miongoni mwa wateja na nilikuwa nimelewa.

Muziki ulikuwa ukipigwa kwa sauti ya juu huku watu wengi wakiwa wanakunywa pombe, kutafuna mirungi, kujidunga madawa ya kulevya na kila aina ya ufuska, huku wengine wakifanya matendo yasiyostahili kufanywa hadharani na wanawake waliokuwa ndani ya grosari hiyo ya aina yake.

Nilichezesha macho kwa kasi kubwa na hatimaye nilifanikiwa kumuona Suma akiwa amekaa na mwanamke mmoja mnene aliyevalia nusu utupu, wakiwa wananyonyana ndimi.

Nikateleza kama nyoka na kumfikia, kufumba na kufumbua tulikuwa tukitazamana naye, ana kwa ana huku bomba la AK47 nikiwa nimelikandamiza kwenye ubavu wake wa kushoto.

“Inuka na ufanye ninachokueleza, ukizingua unajua nini kitatokea,” nilisema kwa sauti ya chini lakini yenye mamlaka, yule mwanamke akakurupuka akiwa ni kama haamini kilichotokea, Suma naye akawa anatetemeka akiwa haelewi nimeingiaje pale.

“Snox! Nakuomba mdogo wangu, please show me some mercy!” (Nionee huruma tafadhali) alisema Suma huku akiwa anatetemeka kuliko kawaida lakini sikumjali.

“Look at my face!” (Nitazame usoni), nilimwambia kwa Kiingereza kilichonyooka, akanitazama usoni halafu akawa ni kama ameshtuka kidogo.

“Mlikuja mkanipiga na kunijeruhi kiasi hiki, mkamteka Saima wangu na kama hiyo haitoshi, mmekuja kuchoma moto nyumba yetu.

Bado unategemea kwamba nitakuonea huruma?” nilisema huku na mimi nikitetemeka kwa hasira.

”No! Nisikilize kwanza Snox,” alisema huku akiniita kwa jina langu la kazi. Watu wengi mitaani huwa wanaamini Snox ni jina langu halisi kwa sababu kila ninakoenda ndilo linalotumika lakini ukweli ni kwamba halikuwa jina langu halisi wala halikuwa na uhusiano wowote na jina langu halisi.

Kiuhalisia jina langu naitwa Keneth au Kenny lakini kama nilivyosema, waliokuwa wakinijua kwa jina hilo, walikuwa wachache mno, tena wale wanaonijua tangu nikiwa mdogo lakini wengine wote walikuwa wakiniita Snox.

“Najua mlitumwa, nataka kujua mhusika ni nani,” nilisema huku nikimkokota taratibu kuelekea kule uani.

 

Yaani ungeshuhudia kilichokuwa kinaendelea, pengine ungepata picha halisi ya kile wanachosema ‘sungura kamkaba tembo’.

Suma alikuwa na mwili mkubwa uliojengeka kimazoezi lakini licha ya ukweli kwamba mimi nilikuwa na kamwili kadogo ka wastani, nilikuwa namkokota kama ng’ombe anayepelekwa machinjioni.

Kwa jinsi nilivyoingia eneo lile mpaka kumpata, bado alikuwa amepigwa na butwaa na hiyo pekee ilitosha kumchanganya kichwa na kibaya alikuwa anafahamu akili zangu nikishika ‘mashine’ zinakuwaje kwani tumewahi kufanya ‘kazi’ pamoja.

“Nataka jibu, sitaki blaah! Blaah!” nilisema huku nikizidi kulikandamiza bomba la AK47 kwenye ubavu wake, nikaikoki na kumfanya ashtuke.

“Nitakwambia Snox, mimi na wewe tumeshakuwa kama ndugu, huna haja ya kutumia nguvu kwangu,” alisema Suma kwa upole, nikatega masikio kwa makini kumsikiliza.

“Mzee anasema umemsaliti, anataka kuhakikisha unapata taabu mpaka mwenyewe ukome.”
“Mzee gani?”

“Aah Snox, kwani nikisema mzee wewe unaelewaje? Kuna mwingine tena zaidi ya bosi?”
“Nimemsaliti kivipi?”

“Kitendo cha kukataa kazi bila sababu za msingi, kimemkasirisha sana na anasema atahakikisha anakomaa na wewe mpaka aone mwisho wako,” alisema Suma lakini maneno yake hayakuniingia akilini.

Nilijua kabisa kwamba ananidanganya kwa sababu alichokisema hakikuwa na uzito wowote wa kumfanya mtu aniwinde kwa kiasi kile.

“Saima yuko wapi?”

“Sijui chochote kuhusu Saima, sikuhusika kwenye hiyo kazi.”

“Unanificha si ndiyo?”

“Snox, sina sababu ya kukuficha chochote ndugu yangu, ila labda Seba anaweza kuwa anajua chochote maana siku hizi ndiyo mtu wa karibu zaidi na mzee.”

“Nitampata wapi?”

“Lazima muda huu atakuwa anakula bata Trace Element, kule Masaki,” alisema Suma akitegemea kwamba baada ya maelezo hayo nitamuachia.

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia:

www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com , Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online. Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

Leave a Comment