
KUELEKEA mchezo wa mkondo wa pili wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya wenyeji Orlando Pirates dhidi ya Simba utakaopigwa leo Jumapili nchini Afrika Kusini, zile fitna zote ambazo ziliwekwa na wapinzani, Simba imezipangua.
Baada ya kufanikiwa katika hilo, uongozi wa Simba umeweka wazi kuwa, wapo tayari kwa mapambano, huku mastaa wa kikosi hicho wakiapa kufanya kila linalowezekana kutinga nusu fainali.
Leo Jumapili majira ya saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, Simba watashuka uwanjani kuvaana na Orlando Pirates katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya mchezo wa kwanza hapa Dar Simba kushinda 1-0.
Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Tunashukuru kwa kusafiri salama mpaka hapa Afrika Kusini, wachezaji wote wako salama licha ya kwamba kuna mazingira ya baridi kali, lakini ni jambo la kawaida kwani tumeshacheza michezo mingi katika hali hii.

“Shauku yetu kubwa ni kuhakikisha tunamaliza tulilolianza nyumbani kwa kufanikisha malengo yetu ya kutinga nusu fainali.
“Mara tu baada ya kuwasili (juzi Ijumaa) kikosi kilianza mazoezi na wachezaji wote wana ari kubwa kuelekea mchezo huu ambapo nimezungumza nao wanaonesha wako tayari kuandika rekodi ya kucheza nusu fainali.”
WAPANGUA FITINA ZOTE
Ofisa mmoja wa Simba aliyesafiri na timu hiyo, aliliambia Spoti Xtra kwamba: “Mpaka sasa hakuna changamoto yoyote tuliyokutana nayo, tulijiandaa kwa lolote ndiyo maana unaona hadi sasa tupo vizuri, kama kuna fitina walituwekea, tumezikwepa. Tunafahamu mechi za ugenini zinakuwa na mambo mengi, hivyo tuna uzoefu nazo, hazitusumbui tena.
“Masuala ya usalama yapo vizuri kabisa, covid-19 tumepima, wote tuko vizuri, hivyo hakuna shida yoyote nje ya uwanja.”
Ikumbukwe kuwa, baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa wikiendi iliyopita jijini Dar, Kocha wa Orlando Pirates, Mandla Ncikazi, alitoa shutuma nzito kwa Simba akisema waliwafanyia vitendo vya kinyama, huku kukiwa na tishio la Simba nao kukutana na hali kama hiyo wakienda Sauzi.
Juzi Ijumaa baada ya kufika Sauzi, Simba walitoa taarifa kwa kusema: “Asanteni Orlando Pirates kwa mapokezi lakini mmetunyima polisi wa kutuongoza barabarani (escort), hivyo tumelazimika kutumia gari la Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kutuongoza.”
MSIKIE PABLO
Akizungumzia mchezo wa leo, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco, amesema: “Tumekuja hapa tukiwa na faida ya bao moja tulilofunga nyumbani, hii ni nzuri kwetu.
“Mchezo wa kesho (leo) tutajitahidi kushinda kwa kufunga angalau bao moja, tuna nafasi ya kufuzu ingawa mchezo utakuwa mgumu, ndoto yetu ni kutinga nusu fainali.”
Kiungo wa timu hiyo, Rally Bwalya, naye alisema: “Tumekuja hapa kushindana, sisi kama wachezaji tunafahamu umuhimu wa mchezo huu ambapo utakuwa mgumu kutokana na Orlando kuwa kwao, lakini tutapambana kwa nguvu zote kuona tunaenda nusu fainali ambayo itakuwa nzuri kwetu.”
SAKHO AITEKA SAUZI
Kuelekea mchezo wa leo, Winga wa Simba, Pape Ousmane Sakho, amekuwa gumzo nchini Afrika Kusini kwa kudaiwa kuwa ndiye mchezaji wa kuchungwa zaidi.
Ofisa Mtendaji wa Orlando Pirates, Floyd Mbele, ameliambia Spoti Xtra kwamba: “Sakho na Morrison (Bernard) walicheza vema katika mchezo wa kwanza, tumesikia Morrison hatakuwepo katika mchezo wa pili, lakini Sakho yupo, hivyo anatakiwa kuchungwa sana.
“Hata kocha aliwazungumzia baada ya kumalizika kwa mchezo wa kwanza juu ya ubora wa wachezaji hao, hivyo lazima tuhakikishe tunakuwa salama dhidi yao, furaha yetu ni kwamba mchezo huu tutakuwa nyumbani.”
STORI: JOEL THOMAS NA MARCO MZUMBE