×

Ufafanuzi Kuhusu Anuani za Makazi na Postikodi na Faida Zake

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Innocent Mungi

WIZARA ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetoa ufafanuzi wa kina kuhusu zoezi linaloendelea la anuani za makazi na postikodi ikiwa ni pamoja na faida ambazo wananchi watazipata baada ya kukamilika kwa zoezi hilo.

 

Akizungumza na Global TV katika Kipindi cha Hoja kwa Hoja kinachoendeshwa na mtangazaji Richard Manyota, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa wizara hiyo, Innocent Mungi ameeleza kwamba zoezi hilo litakapokamilika kwa ufasaha, litarahisisha kwa kiasi kikubwa mambo mengi yenye faida kwa wananchi.

 

Mungi amesema anuani za makazi ni mfumo unaotambulisha mahali mtu anapoishi au anapofanya shughuli zake za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na nyumba anayoishi, mahali anapofanyia shughuli zake pamoja na mambo mengine muhimu.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Innocent Mungi akiwa katika mahojiano na Mwandishi wetu Richard Manyota

Ameongeza kwamba mfumo huo wa anuani za makazi, huwa na utambulisho wa jina la mtaa na namba ya nyumba ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu zikiwemo zile za dharura kama magari ya kubebea wagonjwa na huduma za zimamoto kunapotokea majanga ya moto.

 

Mungi ameongeza kwamba katika nyakati hizi za uchumi wa kigijitali, anuani za makazi zitarahisisha biashara za mtandaoni ambapo mtu atakuwa na uwezo wa kufikishiwa huduma mpaka mlangoni bila usumbufu.

 

Kuhusu postikodi, Mungi amesema ili anuani ya makazi ikamilike, lazima kuwe na postikodi ambayo ni namba maalum zilizogawiwa katika ngazi ya kata zote nchi nzima ambazo zinarahisisha kutambua maeneo yote nchini.

 

“Ili kujua postikodi ya mtaa unaoishi, ni rahisi ambapo unaweza kupata majibu kwa kutumia simu yako ya mkononi kwa kubonyeza namba *152*00# kisha bonyeza namba 3 na kufuata maelekezo ya utambulisho.

 

Mahojiano kamili yanapatikana Youtube, Global TV Online.

Leave a Comment