
MKUU wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila amevunja bodi zote za viongozi wa Vyama vya msingi vya Ushirika 335 vilivyopo katika mkoa huo na kuagiza ndani ya wiki moja ufanyike uchaguzi wa viongozi wengine na wakulima wote wa pamba washiriki kwenye uchaguzi huo.
Mbali na uhamuzi huo, Kafulila ameagiza kuodolewa katika nafasi zao, Maofisa wote wa vyama vya msingi vya Ushirika kwenye Halmashauri zote 6 zilizopo kwenye mkoa huo na kuwekwa Maofisa wengine wapya.
Kafulila ametoa maagizo hayo jana jioni wakati akiongea na waandishi wa habari Ofisini kwake, ambapo ameeleekeza katika uchaguzi mpya wa Viongozi wa Amcos wakulima wote wa pamba washirikia bila kujalisha ni wanachama wa Amcos au siyo wanachama.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa amefikia uhamuzi huo kutokana na kuendelea kuwepo na malalamiko mengi yaliyothibitisha kuwepo kwa mchezo mchafu kati ya AMCOS na Maofisa Ushirika uliosababisha mkulima kutopata bei halisi iliyolipwa na Mnunuzi msimu uliopita wa Pamba.
Aidha alisema kuwa zaidi ya asilimia 30 ya wakulima wa pamba katika mkoa huo wanakosa haki ya kuchagua na kuchaguliwa kwenye uchaguzi wa vyama vya msingi vya ushirika kutokana na kutokuwa wanachama, lakini inapofika wakati wa kuuza pamba wanatakiwa kupeleka kwenye Amcos.
“ Kwa msingi huo, nimeagiza wakulima wote bila kujalisha ni wanachama au hapana, washiriki uchaguzi huo lengo ni kupata viongozi ambao ni sahihi na watalipa wakulima malipo yao halali kama ambavyo pamba itauzwa,” alisema Kafulila.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa viongozi wote wa Amcos zipatazo 335 wanachunguzwa na Taasisi ya kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na mpaka sasa Amcos 189 zimechunguzwa na kubaini uwepo wa madudu huku nyingine zikienedelea kuchunguzwa.
Aliwataka wakulima wa pamba kukaa mkao wa kula, kwani bei ya pamba ya mwaka huu itakuwa kubwa zaidi kuwahi kutokea kwa kipindi cha zaidi ya miaka 30 huku akibainisha mfumo utakaotumika kununua pamba ni soko uhuria.