
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Consolata Ngimbwa akizungumza kwenye mkutano wa makandarasi uliofanyika hivi karibuni mkoani Dodoma
BODI ya Usajili wa Makandarasi (CRB), inatarajia kuwakutanisha makandarasi na wadau mbalimbali wa sekta ya ujenzi mkoani Dodoma kwaajili ya kujadili mchango wa Makandarasi katika Uchumi wa Tanzania.
Mkutano huo wa siku mbili wa mashauriano utafanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center mkoani Dodoma tarehe 12 na 13 mwezi huu.
Kwa mujibu wa Msajili wa Bodi hiyo, Mhandisi Rhoben Nkori mkutano huo utawashirikisha wadau wote wakiwemo waajiri, wataalamu washauri, wahandisi na wabunifu majengo.
Aliwataja wengine kuwa ni wakadiriaji majenzi, watunga sera za uwezeshaji wananchi kiuchumi na wataalamu mbalimbali katika sekta ya ujenzi na kwamba kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Umuhimu na Mchango wa Makandarasi katika uchumi wa Tanzania’.

“Mkutano huu wa mashauriano ambao unafanyika kila mwaka ni muhimu sana kwa maendeleo ya sekta ya ujenzi kwa ujumla wake. Wataalamu wa sekta mbalimbali wanakaribishwa kujisajili mapema ili washiriki katika mkutano,” alisema Mhandisi Nkori
Mhandisi Nkori alitaja mada zitakazotolewa kwenye mkutano huo kuwa ni mchango wa makandarasi katika uchumi wa Tanzania na changamoto zinazoathiri mchango wa makandarasi katika uchumi wa nchi.
Alitaja mada zingine kuwa ni masuala ya kodi ya kuzingatiwa kwa makandarasi ili kuboresha mchango wao katika uchumi wa taifa na fursa katika sheria na kanuni za manunuzi ya umma kuwezesha mchango wa makandarasi wa ndani.
Aidha, alitaja mada zingine zitakazotolewa kuwa ni utatuzi wa migogoro katika ununuzi wa umma na kwamba kwenye mkutano huo pia kutakuwa na maonesho ya teknolojia, huduma na vifaa vya ujenzi.
Akizungumza kuhusu maonesho, Mhandisi Nkori alisema CRB inayakaribisha mashirika na makampuni mbalimbali binafsi na ya umma kwenda kuonesha teknolojia, bidhaa, vifaa na zana za ujenzi.
“Mkutano utakuwa na wadau wengi wa sekta ya ujenzi hivyo tunawakaribisha watu binafsi na mashirika kuja kuonesha bidhaa walizonazo kwa washiriki wa mkutano huu wa mwaka,” alisema Mhandisi Nkori