
NI maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Makete mkoani Njombe Juma Sweda aliyoyatoa wiki moja iliyopita kwa kumuagiza Afisa Tarafa ya Bulongwa kuitisha kikao cha viongozi kata ya Bulongwa na Luwumbu kujadili na kufikia muafaka wa kushirikiana kwenye ujenzi wa Bweni la wavulana Shule ya Sekondari Usililo kata ya Luwumbu.
Diwani wa kata ya Bulongwa Benayo Luvanda amesema hawezi kushiriki ujenzi wa Bweni katika Shule hiyo ambayo inatumiwa na wanafunzi wa kata zote mbili (Bulongwa na Luwumbu) kwa kuwa Bulongwa nao wapo kwenye maandalizi ya kujenga shule yao ya Kata.
“Tulikubaliana na wenzetu wa Luwumbu kwamba Bulongwa tunampango wa kujenga shule yetu na hatuwezi kushiriki Luwumbu ambapo wanapaswa kuongeza nguvu kwa 20% tu”alisema Luvanda.
Mtendaji kata ya Luwumbu Bi. Evelina Sanga amesema makubaliano ya kikao cha mwezi Disemba 2021 ilikuwa ni kuhakikisha viongozi wa kata ya Bulongwa wanaenda kuwashirikisha wananchi wao kuhusu ujenzi wa bweni hilo ili kuwa na nguvu za pamoja.

Lakini mpaka sasa hawajapata majibu yoyote kutoka kwa viongozi wa kata ya Bulongwa kuhusu ushirikishwaji huo na ujenzi wa bweni hilo ulishaanza kwa nguvu za wananchi wa Kata ya Luwumbu pekee wanaochangia asilimia 20 huku Serikali kupitia TASAF ikichangia asilimia 80.
Diwani wa kata ya Luwumbu bwana Felix Kyando amesema anashangaa kuona wananchi wa Kata ya Bulongwa pamoja na Diwani wao hawataki kushiriki ujenzi wa bweni ambapo watoto wengi wanaosoma shuleni hapo wanatoka kata ya Bulongwa, huku akiomuomba Diwani wa Bulongwa kutoa ushirikiano kwenye ujenzi huo.