
RAILA Omolo Odinga; ni mwanasiasa mkubwa mno nchini Kenya akitokea katika familia maarufu ya kisiasa nchini humo.
Kofia ya urais imekuwa ikimpitia kando katika kipindi chote cha miongo kadhaa ya maisha yake ya siasa; kama ilivyomtokea baba yake, Omolo Odinga ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Rais baada ya Kenya kupata uhuru kutoka kwa Waingereza.
Akiwa na umri wa miaka 77 sasa, Odinga anafanya jaribio lake la tano la kuwania Urais katika uchaguzi wa Agosti 9, mwaka huu akiwa amewahi kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 2008; moja ya nafasi za juu za utawala nchini humo.
Odinga ana wafuasi wengi na mashabiki wake wanaomfuatilia kwa karibu wamempa majina kama Baba, Agwambo na Tinga; lililotolewa kutoka kwenye nembo ya chama chake katika uchaguzi wa 1997.
Mtindo wake wa wa kucheza taratibu nyimbo za Reggae wakati wa mikutano yake imepewa jina la Staili au Mtindo wa Kucheza wa Raila.
Odinga sasa anaahidi kuendeleza hoja ya maendeleo ya Rais Uhuru Kenyatta anayemaliza muda wake na kuboresha maisha ya Wakenya walio hatarini kwa kuwapa posho ya shilingi 6,000 za Kenya sawa na Dola za Kimarekani 50 kila mwezi kutoka kwenye hazina mpya ya hifadhi ya jamii, endapo atachaguliwa kuwa Rais.

Pesa za mfuko huo, anasema zitatokana na anachokiita kukabiliana na ufisadi ulioenea nchini humo.
Odinga ameahidi kutoa huduma za afya kwa gharama nafuu kupitia mpango anaouita Baba Care, akijitangaza kama baba katika Taifa hilo lenye watu zaidi ya milioni 56.
Haijulikani kama hili litakuwa jaribio la mwisho la mzee huyo mwenye umri wa miaka 77 katika kuwania Urais.
Awali, Raila alielezea azma yake ya urais mwaka 2017 kama risasi yake ya mwisho, kwa maana ya jaribio lake la mwisho.
Lakini alieleza hatua yake ya kubadilisha maamuzi hayo katika mahojiano na Sophie Ikenye wa BBC Focus on Africa TV mnamo Machi 2022, kwa kueleza kuwa Wakenya walimtaka agombee tena Urais kwa sababu ya imani kubwa waliyonayo kwake.
Odinga amemchagua aliyekuwa Waziri wa Sheria, Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake.
Hili linaonekana ni jambo la kihistoria; ni mara ya kwanza kwa mgombea urais kumchagua naibu mwanamke kwa Kenya kama ilivyokuwa kwa Tanzania mwaka 2015.
Cc; @sifaelpaul