
TIMU ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars imeambulia kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Timu ya Taifa ya Algeria katika mechi ya pili ya kufuzu kushiriki fainali za mataifa ya Afrika AFCON zinazotarajiwa kufanyika mwakani nchini Ivory Coast.
Katika mchezo huo Taifa Stars ilianza kwa kusuasua kipindi cha kwanza kwa wenyeji kutawala sehemu kubwa ya mchezo na bao la dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza lilitosha kuwapeleka Algeria kifua mbele kuelekea mapumziko.

Mabadiliko yaliyofanywa na mwalimu Kim Poulsen kipindi cha pili ya kuwaingiza Kibu Dennis, George Mpole, Kelvin John na Salum Abubakar yalileta matumaini ya kusawazisha bao lakini dakika za majeruhi Algeria walipata bao jingine la pili na hadi kipyenga cha mwisho kinapulizwa na mwamuzi Algeria walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0
Kwa matokeo hayo Kocha Kim Poulsen atakuwa na kazi ya kufanya kuhakikisha anakiandaa kikosi chake ili kiweze kujidhatiti katika michezo mingine inayofuata hasa mchezo dhidi ya majirani zao Uganda.