
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa vijijini 14 vilivyopo katika eneo la Loliondo kutulia kwasababu hakuna kazi yoyote ya kuwaondoa katika maeneo yao.
Akizungumza bungeni leo Ijumaa Juni 9, 2022, Majaliwa amesema kuwa shughuli inayoendelea ambayo ilianza juzi ni kuweka alama (bicon) katika maeneo ambayo yanatakiwa kulinda.
Amesema alama (bicon) zinawekwa katika kulinda mapitio ya wanyama, mazalia ya wanyama na vyanzo vya maji.
Majaliwa amesema eneo linalowekwa liko umbali wa kilometa nane kutoka kijiji ambacho kiko karibu na eneo hilo.
“Eneo hilo liko mbali sana na makazi ya wananchi. Kwa Loliondo hakuna mtu atakayeondolewa katika eneo hilo. Hakuna askari ambaye alikwenda katika kijiji ndio maana ile video huoni askari yeyote,”amesema.
Amesema wapo watu wasiokuwa na nia njema ambao wanataka kutengeneza taswira mbaya ndani na nje ya nchi ndio waliotengeneza video hiyo ikiwaonesha wakazi waeneo hilo wakiwa na mishale.
Kwa upande wake Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameshauri Serikali kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu na mashirika yasiyo ya kiserikali (Ngos) yanaoeneza upotoshaji huo.