
SERIKALI imesema magari yataanza kulipia fedha yanapopita kwenye Daraja la Tanzanite na katika barabara nyingine mbili za haraka ya Kibaha – Mlandizi – Chalinze – Morogoro (Expressway) na ile ya Igawa – Songwe -Tunduma (Expressway) kwa kuwa zote zina sifa za kutozwa fedha.
Katika hotuba ya Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa siku chache zilizopita bungeni Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, alisema serikali inaendelea kuboresha sekta ya uchukuzi nchini kwa kuendeleza utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara ili kufungua fursa za kiuchumi.
Alisema katika kutekeleza miradi hiyo ya ujenzi wa barabara kama sehemu ya kufungua fursa na kuiunganisha nchi na mataifa jirani, serikali itamalizia ujenzi wa barabara zinazounganisha mikoa na kwamba wakandarasi wapo kazini.
Alisema katika ujenzi huo, Daraja la Tanzanite lililopo maeneo ya Salender Dar es Salaam lenye urefu wa kilometa 1.03 lililojengwa baharini jirani na ufukwe wa Coco litawekewa malipo ya fedha kwa sababu lina sifa za kufanya hivyo. Daraja hilo lina njia nne za magari na njia mbili za watembea kwa miguu, limejengwa pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 5.2 na linaunganisha Hospitali ya Aga Khan na barabara za Obama, Kenyatta na Toures mkoani humo na kubadilisha mandhari yake.
Dk Mwigulu alitaja barabara nyingine zitakazowekwa tozo ya barabara kwa sababu zina sifa za kufanywa hivyo ni ile ya Kibaha – Mlandizi – Chalinze – Morogoro ambayo ujenzi wake ukikamilika utakuwa na urefu wa kilometa 158 na Barabara ya Igawa – Songwe -Tunduma ambayo ikikamilika ujenzi wake itakuwa na urefu wa kilometa 218.