
BARCELONA wamefikia makubaliano na Klabu ya Bayern Munich kwa ajili ya kumsajili Robert Lewandowski kwa mkataba wa miaka mitatu.
Mazungumzo hayo yamefikiwa juzi na wakati wowote kutoka sasa Barcelona wakikamilisha utaratibu, watamtangaza rasmi Lewandowski.
Lewandowski alikuwa amesaliwa na mwaka mmoja ndani ya Bayern Munich na alieleza wazi kuwa anataka kuondoka.
Ripoti zinaeleza kuwa, dili hilo limekamilika kwa asilimia kubwa, vilivyosalia ni vichache kabla ya staa huyo kutambulishwa.
Staa huyo raia wa Poland, anatajwa kujiunga na Barcelona kwa euro 45m, huku euro 5m zikiwa nyongeza. Jana Jumamosi Lewandowski alitarajiwa kutua Barcelona kwa ajili ya vipimo.
Imeelezwa kuwa, staa huyo atatambulishwa Barcelona itakaporejea Camp Nou kabla ya mchezo wao maalum wa Joan Gamper Trophy ambao Barcelona watacheza Pumas UNAM, Agosti 7 mwaka huu.
Lewandowski anakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na Barcelona kuelekea msimu ujao baada ya Raphinha, Franck Kessie na Andreas Christensen.