×

Mama wa Kambo Amfungia Mtoto Ndani Siku 3 Bila Chakula, Asingizia Amepotea

Enelesi Mwakalobo Mama wa kambo

MTOTO wa kike Vanessa Mwakalobo miaka 10 mkazi wa Tunduma kata ya majengo mapya amefungiwa ndani ya chumba kwa siku 3 na mama yake mlezi huku akidai mtoto amepotea .

 

Akihojiwa na mwandishi wetu mtoto Vanessa amesema kuwa siku ya jumamosi aliporudi shule alimkuta mama yake mlezi nyumbani ambapo mama huyo alimshika mkono na kwenda kumfungia chumbani bila kumweleza chochote mpaka pale alipokuja kufunguliwa na wenzake wakimwambia kuwa anaitwa na walimu shuleni.

 

Edina Mwakalobo mkazi wa mkoa wa Mbeya ambaye ni Mama mzazi wa mtoto huyo amesema kuwa alipokea taarifa za mtoto kupotea siku ya jumamosi usiku kutoka kwa dada yake ajulikanaye kwa jina la Enelesi Mwakalobo ambaye ndiye mlezi wa mtoto huyo na siku ya jumapili alianza safari ya kwenda kwa dada yake ili wasaidiane kumtafuta mtoto lakini dada yake hakuonyesha ushirikiano na kumtaka mdogo wake asifike nyumbani kwake kwa madai ya kuwa hayupo nyumbani anasafiri kwenda sumbawanga.

Edina Mwakalobo Mama mzazi wa mtoto

Edina aliongeza kwa kusema baada ya kufika Tunduma siku ya juma tatu alifika shuleni anakosoma mtoto na kuomba wanafunzi wanaosoma na Mwanae waende nyumbani kwa dada yake kumpitia Mwanae ndipo walimkuta mfanyakazi wa ndani aliyewaeleza wanafunzi wale kuwa mwenzao amefungiwa chumbani ndipo walimfungulia na kwenda kumkutanisha na mama yake.

 

Alipotafutwa mama mlezi wa mtoto huyo Enelesi Mwakalobo ili kutoa ufafanuzi wa madai ya kumfungia mtoto na kudai kuwa amepotea hakutoa ushirikiano na kusema hawezi kuzungumza chochote kuhusu tukio hilo.

 

Balozi wa Shina namba 6 mtaa wa majengo mapya Zawadi Ngomale Mwasenga anakili kuwepo kwa kadhia hiyo mtaani kwake na kueleza namna walivyoshughulikia ikiwa ni pamoja na kumkabidhi mtoto kwa mama yake mzazi pamoja na kuomba familia ikae chini kutafakari swala hilo kwakua swala hilo ni la ndani ya familia.

Leave a Comment