
KAMATI ya Utendaji ya Klabu ya Yanga ambayo iliketi jana Julai 30, 2022 ilipokea na kujadili pendekezo la Senzo Hammilton Mazingiza la kutokuongeza mkataba wake unaoisha tarehe 30 Julai 2022.
Kamati hiyo imefanya Kikao chake cha kwanza cha kikatiba, Serena Hotel jijini Dar es salaam chini ya uenyekiti wa Rais wa Klabu Eng. Hersi Ally Said.
Senzo aliwasilisha ombi hilo lenye muktadha wa sababu za kifamilia ambayo amekuwa nayo mbali kwa kipindi cha takribani miaka mitatu.
Ombi hilo limepokelewa na baada ya kujadiliwa, Kamati ya utendaji ilikubali ombi hilo na kumteua wakili Simon Patrick kuwa Afisa mtendaji Mkuu wa Mpito(Interim Chief Executive Officer).
Aidha Yanga inamshukuru Bw. Senzo kwa utumishi wake ulio bora hasa katika mchango wake kwenye eneo la utawala na kumtakia kila la heri.
