
NCHI za China na Taiwan zimeingia katika mgogoro mkubwa wa kibiashara kufuatia ziara ya Spika wa Bunge la Congress la Marekani Nancy Pelosi.
Mamlaka ya Biashara na Wateja ya China imesitisha usafirishwaji wa mchanga kwenda Taiwan ambao ni malighafi muhimu kwa ajili ya shughuli za ujenzi, lakini pia imesistisha uingizwaji wa bidhaa za matunda kamavile machungwa, malimao na ndimu sambamba na baadhi ya aina ya samaki kutoka Taiwan.

Mamlaka ya Biashara nchini China imeziweka kikaangoni baadhi ya kampuni za vyakula kutoka Taiwan ambazo bado hazijakamilisha usajili wa vibali vya kusafirisha bidhaa nje ya nchi yao.
Wu Shou- Mei, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini Taiwan amebainisha kuwa maamuzi hayo yaliyochukuliwa haraka yanaweza kuwa yamesababishwa na mtazamo wa kisiasa kutokana na makampuni ya Taiwan kuhudumiwa tofauti na makampuni ya mataifa mengine.
Nchi ya China ndiyo mfanyabiashara mwenza mkuu wa Taiwan, Kisiwa hicho kimesafirisha bidhaa kwenda China na Hong Kong ambapo imetengeneza zaidi ya Dola Bilioni 188.9 kwa mwaka 2021.