
ADHA ya usafiri imetokea kwa wasafiri wanaofanya safari zao kati ya Morogoro-Dar es Salaam baada ya Lori lililobeba magogo kushindwa kupanda mlima na hatimaye kufunga barabara katika eneo la Mikese Morogoro na kusababisha foleni kubwa.
Taarifa zinadai kuwa adha hiyo ilianza usiku wa kuamkia leo huku ikisababisha usumbufu kwa mamia ya wasafiri ambao walikadiriwa kusafiri kwa zaidi ya masaa saba.

Fortunatus Muslimu ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro tayari ameshafika eneo la tukio na amebainisha kuwa juhudi za kutatua changamoto hiyo zinafanyika ikiwa ni pamoja na kutafuta nyenzo ya kupunguza magogo ili kusogeza gari kando ya barabara na kupisha magari yapite.
Aidha Kamanda Muslimu amesema kuwa tayari zoezi la kuruhusu baadhi ya magari yapite limefanikiwa huku akisisitiza kwa kutoa rai kwa watumiaji wengine wa barabara kuwa na subiri wakati juhudi za kutatua adha hiyo zinafanyika.