
KOCHA Mkuu wa Polisi Tanzania, Joslin Sharif, amefunguka kuwa, tayari amezungumza na mabeki wake ili kuhakikisha hawafanyi makosa na kuadhibiwa na straika wa Yanga, Fiston Mayele.
Kauli ya kocha huyo imekuja wakati leo Jumanne Polisi Tanzania itakuwa mwenyeji wa Yanga kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu kwa timu hizo ukitarajiwa kuchezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Akizungumza na Spoti Xtra, Joslin alisema: “Tunamshukuru Mungu kikosi kipo salama na morali ni kubwa kuelekea kwenye mchezo wetu wa kwanza dhidi ya Yanga.
“Tunatambua umuhimu wa huo mchezo na tumeona wapinzani wetu wana kikosi kizuri, lakini hata sisi tumesajili wachezaji wazuri, hivyo tuna imani wataenda kupambana.

“Mayele ni mchezaji mzuri na anajua kufunga, lakini ana miguu miwili kama wachezaji wetu, hivyo tutacheza naye kwa tahadhari.
“Nimewafundisha mabeki wangu na kuwaambia kwamba wasifanye makosa yale ambayo yatasababisha kupoteza mchezo kama ule wa msimu uliopita, hivyo nina imani wataenda kuyatekeleza.”
Mapema jana, msafara wa wachezaji 25 wa Yanga, ulifika jijini Arusha kutoka Dar tayari kwa mchezo huo.
Akizungumza na Spoti Xtra, Kocha Msaidizi wa Yanga, Cerdic Kaze, alisema: “Tumesafiri na wachezaji wote tuliowasajili akiwemo Kambole (Lazarous) ambaye alikosekana katika mchezo wa dabi kutokana na majeraha aliyoyapata.
“Kambole amepata nafuu ya majeraha yake, hivyo huenda akawa sehemu ya wachezaji watakaocheza mchezo huo.
“Hivyo niwatake mashabiki wetu wa Yanga wajitokeze kwa wingi uwanjani kwa ajili ya kuisapoti timu yao kama walivyofanya katika dabi na msimu uliopita tukienda kutetea ubingwa wetu wa ligi. Tunawaahidi kuendelea pale tulipoishia.”
STORI NA LEEN ESSAU NA WILBERT MOLANDI