
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolph Mkenda, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya tatu ya wanafunzi waliosoma vyuo vikuu nje ya nchi yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya wakala wa vyuo vikuu nje ya nchi, Global Education Link (GEL), Abdlulmalik Mollel, wakati akizungumzia mahafali hayo.
Alisema hayo ni mahafali ya wanafunzi waliobahatika kusoma nje ya nchi na kuhitimu yatakayofanyika siku ya Jumapili katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam kuanzia asubuhi.
Alisema mabalozi wanchi mbalimbali ambazo vijana hao wamesoma wamethibitisha kushiriki katika mahafali hayo.
Alisema kwenye mahafali hayo wamealika Wizara ya Mmabo ya Nje, Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu Zanzibar na Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU).
Alisema wengine waliothibitisha kushiriki ni Bodi ya Tiba Tanganyika (MCT), Bodi ya Uhasibu (NBAA), Sekretarieti ya Ajira ambayo ilikuwa ikitoa mafunzo kwa wahitimu kuhusu namna ya kujiajiri wanapomaliza masomo badala ya kusubiri kuajiriwa.
“Ili mahafali haya yafane mlengwa mkubwa ni mzazi na mtoto wake kwasababu mwanafunzi aliyesoma nje anakuja kusherehekea na wazazi na walezi waliojinyima kumlipia ada hivyo wanafunzi wametibitisha kushiriki,” alisema
Mollel alisema wanafunzi wanaotarajia kwenda nje ya nchi kusoma wataalikwa ili waweze kujifunza kutimiza malengo yao kama wenzao walioenda kusoma wakahitimu na wakarudi nyumbani kuleta ujuzi kusaidia maendeleo ya nchi yao.
Alisema wanafunzi wa Kitanzania watakaokwenda nje ya nchi watabebeshwa malengo ya kuitangaza nchi ili kusaidia jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akiitangaza nchi kwenye maeneo mbalimbali duniani.
“Tunamwona mama yetu anavyokwenda nje ya nchi yetu kuisemea katika rasilimali tulizonazo, fursa na uzuri wanchi yetu sasa peke yake hataweza tunataka watanzania watakaokwenda nje sasa hivi kuitangaza nchi liwe ajenda ya kipaumbele,” alisema Mollel
Alisema anataka kuona mwanafunzi anayekwenda nje ya nchi anaporudi anarudi na wawekezaji kwenye nyanja mbalimbali kama elimu na utalii badala ya kuhitimu na kurejea nchini wakiwa na vyeti vitupu.